Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Samueli 19 - Swahili Revised Union Version

1 Kisha Yoabu akaambiwa, Angalia, mfalme anamlilia Absalomu na kumwombolezea.

2 Na kushinda kwao vitani siku ile kukageuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote; maana watu walisikia siku ile ya kwamba, Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.

3 Watu wakajificha siku ile, wakaingia mjini kama vile watu waonao fedheha wajifichavyo, hapo wakimbiapo vitani.

4 Mfalme akajifunika uso; na mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu!

5 Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wake zako, na roho za masuria wako;

6 kwa kuwa unawapenda wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angalikuwa hai, na sisi sote tungalikuwa wafu leo, ingekuwa vyema machoni pako.

7 Basi sasa, ondoka, utoke nje, ukaseme na watumishi wako maneno ya kuwatuliza roho zao; maana mimi nakuapia kwa BWANA, usipotoka, hatabaki hata mtu mmoja pamoja nawe usiku huu; na mambo haya yatakuwa mabaya kwako kuliko mabaya yote yaliyokupata tokea ujana wako hadi sasa.

8 Ndipo mfalme akaondoka, akaketi langoni. Nao wote wakaambiwa ya kwamba, Angalieni, mfalme ameketi langoni; watu wote wakaenda huko mbele ya mfalme. Basi, Israeli wote walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake.


Daudi aitwa kurudi Yerusalemu

9 Wakashindana watu wote katika kabila zote za Israeli, wakisema, Mfalme alitutoa mikononi mwa adui zetu, akatuokoa mikononi mwa Wafilisti; naye sasa amekimbia kutoka nchi hii kwa sababu ya Absalomu.

10 Na huyo Absalomu, tuliyemtia mafuta ili awe juu yetu, amekufa vitani. Basi sasa mbona ninyi hamsemi neno lolote juu ya kumrudisha tena mfalme?

11 Naye mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na Abiathari, makuhani, kusema, Neneni na wazee wa Yuda, mkisema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme nyumbani kwake? Kwa maana maneno ya Israeli wote yamemjia mfalme, ili kumleta nyumbani kwake.

12 Ninyi ni ndugu zangu, ninyi ni mfupa wangu na nyama yangu; mbona basi ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme?

13 Kisha mkamwambie Amasa, Je! Si wewe uliye mfupa wangu, na nyama yangu? Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, usipokuwa wewe jemadari wa jeshi mbele yangu daima mahali pa Yoabu.

14 Akawainamisha mioyo watu wote wa Yuda, kama mtu mmoja; basi wakatuma kwa mfalme, Rudi wewe na watumishi wako wote.

15 Hivyo mfalme akarudi, akafika Yordani. Kisha watu wa Yuda wakaja Gilgali kumlaki mfalme, na kumvusha mfalme Yordani.

16 Akafanya haraka Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu akashuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi.

17 Na Watu elfu moja wa Benyamini walikuwa pamoja naye, na huyo Siba mtumishi wa nyumba ya Sauli, na hao wanawe kumi na watano, na watumishi wake ishirini pamoja naye; wakavuka Yordani mbele ya mfalme.

18 Tena ikavuka mashua ili kuwavusha jamaa ya mfalme, na kufanya aliyoyaona kuwa mema. Ndipo Shimei, mwana wa Gera, akamwangukia mfalme alipokuwa amevuka Yordani.


Daudi amsamehe Shimei

19 Akamwambia mfalme, Bwana wangu asinihesabie uovu, wala usiyakumbuke yale niliyoyatenda mimi mtumishi wako kwa upotovu siku ile alipotoka Yerusalemu bwana wangu mfalme, hata mfalme ayatie moyoni mwake.

20 Kwa kuwa mimi mtumishi wako ninajua ya kwamba nimekosa; kwa hiyo, tazama, nimekuja leo, wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu, kushuka ili nimlaki bwana wangu mfalme.

21 Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akajibu na kusema, Je! Shimei hatauawa kwa sababu hii, kwa kuwa amemlaani masihi wa BWANA?

22 Lakini Daudi akasema, Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya, hata mmekuwa adui zangu leo? Je! Atauawa mtu yeyote leo katika Israeli? Kwa maana sijui mimi leo ya kwamba ndimi mfalme juu ya Israeli?

23 Kisha mfalme akamwambia Shimei, Hutakufa. Mfalme akamwapia.


Daudi na Mefiboshethi wakutana

24 Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hadi siku hiyo aliporudi kwake kwa amani.

25 Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi?

26 Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumishi wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumishi wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumishi wako ni kiwete.

27 Naye amenisingizia mimi mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako.

28 Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumishi wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi?

29 Basi mfalme akamwambia, Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi.

30 Naye Mefiboshethi akamwambia mfalme, Naam, hata yote na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake.


Wema wa Daudi kwa Barzilai

31 Tena Barzilai, Mgileadi, akashuka kutoka Rogelimu; akavuka Yordani pamoja na mfalme, amvushe Yordani.

32 Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, alikuwa na umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa.

33 Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu.

34 Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Nina miaka mingapi ya kuishi, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu?

35 Sasa nina miaka themanini; nami je! Naweza kupambanua mema na mabaya? Mimi mtumishi wako, je! Naweza kuonja nilacho au ninywacho? Naweza kusikia tena sauti ya waimbaji wa kiume na wa kike? Kwa nini basi mtumishi wako azidi kumlemea bwana wangu mfalme?

36 Mtumishi wako ataka kuvuka Yordani tu pamoja na mfalme; tena mbona mfalme anilipie thawabu ya namna hii?

37 Niache nirudi basi, mimi mtumishi wako, ili nife katika mji wangu mwenyewe, karibu na kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, mtumishi wako Kimhamu; na avuke yeye pamoja na bwana wangu mfalme; nawe ukamtendee yeye yaliyo mema machoni pako.

38 Mfalme akajibu, Haya, Kimhamu na avuke pamoja nami, nami nitamtendea yaliyo mema machoni pako wewe; na kila utakalotaka kwangu, mimi nitalifanya kwa ajili yako.

39 Basi watu wote wakavuka Yordani, naye mfalme akavuka; kisha mfalme akambusu Barzilai, akambariki; naye akarudi nyumbani kwake.

40 Hivyo mfalme akavuka, akafika Gilgali; Kimhamu akavuka pamoja naye; na watu wote wa Yuda wakamvusha mfalme, na nusu ya watu wa Israeli.

41 Tena, angalia, watu wote wa Israeli wakamjia mfalme wakamwambia mfalme, Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda wamekuiba, na kumvusha Yordani mfalme, na jamaa yake, na watu wote wa Daudi pamoja naye?

42 Ndipo watu wote wa Yuda wakawajibu hao watu wa Israeli, Ni kwa sababu mfalme ni wa jamaa yetu; mbona basi ninyi mmekasirika kwa ajili ya jambo hili? Je! Sisi tumekula kitu cha mfalme? Ama ametupa sisi zawadi yoyote?

43 Hao watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, wakasema, Sisi tunazo sehemu kumi katika mfalme, tena tunayo haki yetu katika Daudi zaidi kuliko ninyi; mbona basi ninyi mmetudharau sisi, msitake ushauri wetu kwanza katika kumrudisha tena mfalme wetu? Na maneno ya watu wa Yuda yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo