Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

1 Wafalme 11 - Swahili Revised Union Version


Makosa ya Sulemani

1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti,

2 na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.

3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wake zake wakamgeuza moyo.

4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.

5 Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu wa kike wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni.

6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, wala hakumfuata BWANA kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.

7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni.

8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.

9 Basi BWANA akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha BWANA, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,

10 akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru BWANA.

11 Kwa hiyo BWANA akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.

12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.

13 Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.


Adui za Sulemani

14 Ndipo BWANA akamwinulia Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; aliyekuwa wa wazawa wake mfalme wa Edomu.

15 Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu,

16 (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hadi alipompoteza kila mwanamume wa Edomu);

17 yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi angali ni mtoto mdogo.

18 Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akaamuru apewe vyakula, akampa mashamba.

19 Hadadi akapendeza sana machoni pa Farao, hata akamwoza dada ya mkewe, dada ya Tapanesi aliyekuwa malkia.

20 Naye huyo dada ya Tapanesi akamzalia Genubathi mwanawe, ambaye Tapanesi alimlea nyumbani mwa Farao; naye Genubathi akawako nyumbani mwa Farao pamoja na wana wa Farao.

21 Naye Hadadi aliposikia huko Misri ya kuwa Daudi amelala na babaze, na Yoabu, jemadari wa jeshi, amekufa, Hadadi akamwambia Farao, Unipe ruhusa, niende mpaka nchi yangu.

22 Farao akamwambia, Umekosa nini kwangu, hata, tazama, unatafuta kuirudia nchi yako? Akajibu, Hakuna, lakini unipe ruhusa tu.

23 Tena, Mungu akamwinulia adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba,

24 naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski.

25 Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.


Uasi wa Yeroboamu

26 Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akamwasi mfalme.

27 Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwasi mfalme. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi.

28 Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii, akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu.

29 Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani.

30 Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili.

31 Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe makabila kumi,

32 (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya makabila ya Israeli);

33 kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake.

34 Lakini sitauondoa ufalme wote katika mkono wake; bali nitamfanya awe mkuu siku zote za maisha yake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi niliyemchagua kwa maana alizishika amri zangu na sheria zangu,

35 ila nitauondoa ufalme katika mkono wa mwanawe, nami nitakupa wewe makabila kumi.

36 Nami nitampa mwana wake kabila moja, ili Daudi, mtumishi wangu, apate kuwa na taa siku zote mbele zangu katika Yerusalemu, mji ule niliouchagua niweke jina langu huko.

37 Nami nitakutwaa wewe, nawe utatawala kama roho yako inavyotamani, nawe utakuwa mfalme juu ya Israeli.

38 Tena itakuwa, ukiyasikia yote nitakayokuamuru, na kuenda katika njia zangu, na kutenda yaliyo mema machoni pangu, ili kuzishika amri zangu na hukumu zangu kama Daudi mtumishi wangu alivyotenda, basi, nitakuwa pamoja nawe, nitakujengea nyumba iliyo imara, kama nilivyomjengea Daudi, nami nitakupa wewe Israeli.

39 Tena nitawatesa wazao wa Daudi kwa sababu hii, lakini si daima.

40 Basi Sulemani akataka kumwua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akaondoka, akakimbilia Misri, kwa Shishaki, mfalme wa Misri, akakaa katika Misri hata wakati wa kufa kwake Sulemani.


Kufa kwa Sulemani

41 Nayo yaliyosalia ya Sulemani, mambo yake na yote aliyoyafanya, na hekima yake, je! Hayo siyo yaliyoandikwa kitabuni mwa mambo yake Sulemani?

42 Na siku alizotawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote zilikuwa miaka arubaini.

43 Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi baba yake; na Rehoboamu mwanawe akatawala mahali pake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo