Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mwanzo 7 - Swahili Revised Union Version


Gharika kuu

1 BWANA akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.

2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, wa kiume na wa kike; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, wa kiume na wa kike.

3 Tena katika ndege wa angani saba saba, wa kike na wa kiume; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote.

4 Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arubaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali.

5 Nuhu akafanya kama vile BWANA alivyomwamuru.

6 Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi.

7 Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika.

8 Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi,

9 wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kike na wa kiume, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu.

10 Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi.

11 Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka.

12 Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arubaini mchana na usiku.

13 Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye;

14 wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yoyote.

15 Waliingia katika safina alimokuwa Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake.

16 Na walioingia, waliingia wa kike na wa kiume, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia.

17 Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arubaini; nayo maji yakazidi, yakaifanya safina ielee, ikaelea juu ya nchi.

18 Maji yakaongezeka zaidi juu ya nchi; na safina ikaelea juu ya uso wa maji.

19 Maji yakazidi kuongezeka sana sana juu ya nchi; hata milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikwa.

20 Maji yakaongezeka hata milima ikafunikwa kiasi cha dhiraa kumi na tano.

21 Wakafa watu wote waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu;

22 kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu.

23 Kila kilichokuwa hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali; mwanadamu, wanyama wa kufugwa, kitambaacho na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao waliokuwa pamoja naye katika safina.

24 Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo