Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mika 1 - Swahili Revised Union Version

1 Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Mika, Mmoreshathi, katika siku za Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; maono aliyoyaona kuhusu Samaria na Yerusalemu.


Hukumu yatangazwa juu ya Samaria

2 Sikilizeni, enyi watu wa kabila zote; sikiliza, Ee dunia, na vyote vilivyomo; Bwana MUNGU na ashuhudie juu yenu, yeye Bwana kutoka hekalu lake takatifu.

3 Kwa maana, angalieni, BWANA anakuja akitoka mahali pake, naye atashuka, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka.

4 Na hiyo milima itayeyuka chini yake, nayo mabonde yatapasuliwa, kama vile nta iliyo mbele ya moto, kama maji yaliyomwagika katika mteremko.

5 Kwa sababu ya kosa la Yakobo yametokea haya yote, na kwa sababu ya makosa ya nyumba ya Israeli. Nini kosa la Yakobo? Je, silo Samaria? Na nini mahali pa Yuda palipoinuka? Sipo Yerusalemu?

6 Kwa ajili ya hayo nitafanya Samaria kuwa kama chungu katika shamba, na kama miche ya shamba la mizabibu; nami nitayatupa mawe yake bondeni, nami nitaifunua misingi yake.

7 Na sanamu zake zote za kuchonga zitapondwapondwa, na ijara zake zote zitateketezwa kwa moto, na sanamu zake zote nitazifanya ukiwa; kwa kuwa amezikusanya kwa ujira wa kahaba, nazo zitaurudia ujira wa kahaba.


Maangamizi ya miji ya Yuda

8 Kwa ajili ya hayo nitaomboleza na kulia, Nitakwenda nimevua nguo, nikiwa uchi; Nitaomboleza kama mbweha, Na kulia kama mbuni.

9 Kwa maana majeraha yake hayaponyeki; Maana msiba umeijia hata Yuda, Unalifikia lango la watu wangu, Naam, hata Yerusalemu.

10 Msiyahubiri haya katika Gathi, msilie kamwe; Katika Beth-le-Afra ugaegae mavumbini.

11 Piteni; njia yenu, wakazi wa Shafiri, mkiwa uchi na wenye aibu; Wakazi wa Saanani msitokeze nje; Beth-eseli unalia na ataondoa msaada wake kwenu;

12 Maana wakazi wa Marothi wanasubiri kwa hamu kupata mema; Lakini maangamizi yameshuka toka kwa BWANA, Yamefika katika lango la Yerusalemu.

13 Mfungie gari la vita farasi Aliye mwepesi, wakazi wa Lakishi; Alikuwa mwanzo wa dhambi kwa binti Sayuni; Maana makosa ya Israeli yameonekana kwako.

14 Kwa hiyo mtaipa Moresheth-Gathi zawadi ya kuagia; Nyumba za Akzibu zitakuwa kijito kidanganyacho wafalme wa Israeli.

15 Bado, wakazi wa Maresha, nitawaleteeni tena yeye atakayewamiliki; Utukufu wa Israeli utafika Adulamu.

16 Jinyoeni upara, jikateni nywele zenu, Kwa ajili ya watoto waliowafurahisha; Panueni upara wenu kama tai; Kwa maana wamekwenda mbali nanyi uhamishoni.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo