Matendo 9 - Swahili Revised Union VersionKuongoka kwa Sauli 1 Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, 2 akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, wanaume kwa wanawake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. 3 Wakati alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafla nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. 4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona wanitesa? 5 Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayemtesa. 6 Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. 7 Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, waliisikia sauti, lakini hawakuona mtu. 8 Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. 9 Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. 10 Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. 11 Bwana akamwambia, Simama, nenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; 12 naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. 13 Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; 14 hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. 15 Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. 16 Maana nitamwonesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu. 17 Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. 18 Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa; 19 akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadhaa pamoja na wanafunzi walioko Dameski. Sauli ahubiri katika Dameski 20 Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. 21 Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaua walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? 22 Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. Sauli aokoka kuuawa na Wayahudi 23 Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue; 24 lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua. 25 Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimteremsha katika kapu. Sauli akiwa Yerusalemu 26 Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. 27 Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. 28 Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. 29 Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kigiriki. Nao wakajaribu kumwua. 30 Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakamtuma aende Tarso. 31 Basi kanisa likapata raha kote katika Yudea na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. Kuponywa kwa Ainea 32 Wakati Petro alipokuwa akizungukazunguka pande zote akawateremkia na watakatifu waliokaa Lida. 33 Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo alikuwa amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. 34 Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; inuka, ujitandikie. Mara akainuka. 35 Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana. Petro akiwa Lida na Yafa 36 Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. 37 Ikawa siku zile akaugua, akafa; wakati walipokwisha kumwosha, wakamweka ghorofani. 38 Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi waliosikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Njoo kwetu pasipo kukawia. 39 Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu ghorofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. 40 Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, inuka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. 41 Akampa mkono, akamwinua; hata kisha akawaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, akiwa hai. 42 Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana. 43 Basi Petro akakaa siku kadhaa huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya