Hosea 4 - Swahili Revised Union VersionMungu ailaumu Israeli 1 Lisikieni neno la BWANA, enyi wana wa Israeli; kwa maana BWANA ana shutuma nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi. 2 Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na kumwaga damu mfululizo. 3 Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa porini na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataangamizwa. 4 Lakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani. 5 Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako. 6 Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako. 7 Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu. 8 Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao. 9 Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao. 10 Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia BWANA. Uzinzi wa Israeli 11 Uzinzi na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. 12 Watu wangu hutaka shauri kwa kipande cha mti, na fimbo yao huwatolea uaguzi; maana roho ya uzinzi imewapotosha, wakawacha Mungu wao. 13 Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati. 14 Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia. 15 Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo BWANA. 16 Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye malisho mazuri. 17 Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. 18 Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. 19 Upepo umemfunika kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya