Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hesabu 14 - Swahili Revised Union Version


Watu wanaasi

1 Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.

2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.

3 Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe kiongozi, tukarudi Misri.

5 Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko la wana wa Israeli.

6 Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao;

7 wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu.

8 Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali.

9 Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; kinga iliyokuwa juu yao imeondolewa, naye BWANA yuko pamoja nasi; msiwaogope.

10 Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.

11 BWANA akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hadi lini? Wasiniamini hadi lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.

12 Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao.


Musa awaombea watu kwa Mungu

13 Basi Musa akamwambia BWANA, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao;

14 kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii; wamesikia wao ya kuwa wewe BWANA u kati ya watu hawa; maana, wewe BWANA waonekana uso kwa uso, na wingu lako lasimama juu yao, kisha wewe watangulia mbele yao, katika nguzo ya wingu mchana, na katika nguzo ya moto usiku.

15 Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena na kusema,

16 Ni kwa sababu yeye BWANA hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani.

17 Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema,

18 BWANA ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yoyote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne.

19 Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa.

20 BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa;

21 lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA;

22 kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu;

23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;

24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye amenifuata kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na wazao wake wataimiliki.

25 Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu.


Ukaidi wa Waisraeli na kushindwa kwao

26 Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

27 Je! Nivumilie na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hadi lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo.

28 Waambieni, Kama niishivyo, asema BWANA, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi;

29 mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia,

30 hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliapa kwa kuinua mkono wangu, kwamba nitawafanyia makao humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

31 Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi mliyoikataa ninyi.

32 Lakini katika habari zenu, maiti zenu zitaanguka katika jangwa hili.

33 Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arubaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hadi maiti zenu zitakapoangamia jangwani.

34 Kwa jumla ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arubaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arubaini, nanyi mtakujua kuchukizwa kwangu.

35 Mimi BWANA nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko watakakokufa.

36 Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung'unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi,

37 watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya BWANA.

38 Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi.

39 Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli wote maneno haya, na hao watu wakaomboleza sana.

40 Wakainuka na mapema asubuhi, wakakwea juu ya mlima hata kileleni, wakisema, Tazameni, sisi tupo hapa, nasi tutakwea kwenda mahali BWANA alipotuahidi; kwani tumefanya dhambi.

41 Musa akawaambia, Kwa nini ninyi sasa kuyakaidi maagizo ya BWANA? Maana halitafanikiwa jambo hilo.

42 Msikwee, kwa kuwa BWANA hayumo kati yenu; msipigwe na kuangushwa mbele ya adui zenu.

43 Kwa kuwa Mwamaleki na Mkanaani wako mbele yenu, nanyi mtaanguka kwa upanga, kwa sababu mmerudi nyuma msimfuate BWANA, kwa hiyo BWANA hatakuwa pamoja nanyi.

44 Lakini walithubutu kukwea mlimani hata kileleni; ila sanduku la Agano la BWANA halikutoka humo kambini, wala Musa hakutoka.

45 Ndipo Mwamaleki, na Mkanaani waliokaa huko mlimani, wakateremka, wakawapiga na kuwaangusha, hadi wakafika Horma.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo