Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Amosi 2 - Swahili Revised Union Version

1 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Moabu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu aliichoma moto mifupa ya mfalme wa Edomu hata ikawa chokaa; Sef 2:8-11; 2 Fal 3:27

2 lakini nitatuma moto juu ya Moabu, nao utayateketeza majumba ya Keriothi; na Moabu atakufa pamoja na mshindo, na kelele, na sauti ya tarumbeta;

3 nami nitamkatilia mbali mwamuzi atoke kati yake, nami nitawaua wakuu wake pamoja naye, asema BWANA.


Hukumu kwa Yuda

4 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA; wala hawakuzishika amri zake; na maneno yao ya uongo yamewakosesha, ambayo baba zao waliyafuata;

5 lakini nitatuma moto juu ya Yuda, nao utayateketeza majumba ya Yerusalemu. Hukumu kwa Israeli.

6 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu;

7 nao hukanyaga vichwa vya maskini katika mavumbi ya nchi na kuwasukuma walioteseka kutoka kwa njia yao; na mtu na baba yake wanamwendea mwanamke mmoja, na kulitia unajisi jina langu takatifu;

8 nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha.

9 Lakini nilimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini niliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini.

10 Pia niliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arubaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori.

11 Nami nikawainua watu miongoni mwa wana wenu wawe manabii, na katika vijana wenu wawe Wanadhiri; je! Sivyo hivyo, enyi wana wa Israeli? Asema BWANA.

12 Lakini mliwapa Wanadhiri mvinyo wanywe; mkawaamuru manabii, mkisema, Msifanye unabii.

13 Tazameni, nitawalemea ninyi, Kama gari lilemeavyo lililojaa miganda.

14 Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake;

15 Wala apindaye upinde hatasimama; Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake;

16 Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa Atakimbia uchi siku ile, asema BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo