2 Samueli 7 - Swahili Revised Union VersionAgano la Mungu na Daudi 1 Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, 2 mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. 3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yuko pamoja nawe. 4 Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, 5 Nenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? 6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. 7 Mahali kote nilikokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lolote na mtu yeyote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? 8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nilikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; 9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. 10 Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; 11 naam, kama ilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. 12 Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. 13 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele. 14 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; 15 lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. 16 Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitaimarishwa milele. 17 Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi. Ombi la Daudi 18 Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? 19 Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumishi wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU. 20 Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumishi wako, Ee Bwana MUNGU. 21 Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumishi wako. 22 Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee BWANA Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. 23 Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao. 24 Nawe ulijifanyia imara watu wako wa Israeli, wawe watu wako milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. 25 Basi sasa, Ee BWANA Mungu, neno lile ulilolinena kuhusu mtumishi wako, na kuhusu nyumba yangu, uliimarishe milele, ukatende kama ulivyosema. 26 Jina lako na litukuzwe milele, kwa kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumishi wako, Daudi, itaimarika mbele zako. 27 Kwa kuwa wewe, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumishi wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumishi wako, nimepata ujasiri nikuombe ombi hili. 28 Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumishi wako jambo hili jema 29 basi, sasa, uwe radhi, ukaibariki nyumba ya mtumishi wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumishi wako na ibarikiwe milele. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya