Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Samueli 21 - Swahili Revised Union Version


Daudi ajilipiza kwa Wagibeoni

1 Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.

2 Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akajaribu kuwaua kwa ari kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;)

3 basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa BWANA?

4 Na hao Wagibeoni wakamwambia, Si jambo la fedha wala dhahabu lililo kati ya sisi na Sauli, au nyumba yake; wala si juu yetu kumwua mtu yeyote katika Israeli. Akasema, Mtakayonena, ndiyo nitakayowatendea ninyi.

5 Wakamwambia mfalme, Yule mtu aliyetupoteza, na kutufanyia shauri la kutuharibu, tusikae katika mipaka yoyote ya Israeli,

6 basi, na tutolewe watu saba katika wanawe, nasi tutawatundika mbele za BWANA katika Gibeoni, katika mlima wa BWANA. Mfalme akasema, Nitawatoa.

7 Lakini mfalme akamwachilia Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo cha BWANA kilichokuwa kati yao, yaani, kati ya Daudi na Yonathani, mwana wa Sauli.

8 Ila mfalme akawatwaa hao wana wawili wa Rispa, binti Aya, aliomzalia Sauli, Armoni na Mefiboshethi; na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliomzalia Adrieli, mwana wa Barzilai, Mmeholathi;

9 akawatia mikononi mwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele za BWANA, nao wakaangamia wote saba pamoja; wakauawa siku za mavuno, za kwanza, mwanzo wa mavuno ya shayiri.

10 Naye Rispa, binti Aya, akatwaa nguo ya magunia akajitandikia mwambani, tangu mwanzo wa mavuno hadi waliponyeshewa mvua toka mbinguni; wala hakuacha ndege wa angani kukaa juu yao mchana, wala wanyama wa mwitu usiku.

11 Kisha Daudi akaambiwa hayo aliyoyafanya huyo Rispa binti Aya, suria wa Sauli.

12 Akaenda Daudi, akaitwaa mifupa ya Sauli na mifupa ya Yonathani mwanawe mikononi mwa watu wa Yabesh-gileadi; waliyoiiba katika njia ya Beth-sheani, hapo Wafilisti walipowatungika, katika siku hiyo waliyomwua Sauli huko Gilboa;

13 naye akaileta toka huko hiyo mifupa ya Sauli, na mifupa ya Yonathani mwanawe; nao wakaizoa mifupa yao waliotundikwa.

14 Kisha wakaizika mifupa ya Sauli na ya Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Zela, kaburini mwa Kishi babaye; wakafanya yote aliyoyaamuru mfalme. Na baadaye Mungu aliiridhia hiyo nchi.


Ushujaa wa jeshi la Daudi

15 Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israeli; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti; naye Daudi akaishiwa na nguvu.

16 Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmoja wa Warefai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani, naye amejifungia upanga mpya, alijaribu kumwua Daudi.

17 Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli.

18 Ikawa baada ya hayo, kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, aliyekuwa mmoja wa Warefai.

19 Kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; na Elhanani, mwana wa Yairi, Mbethlehemi, alimwua Goliathi, Mgiti, ambaye mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mpini wa mfuma nguo

20 Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambako kulikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake ishirini na vinne; yeye naye alizaliwa kwa Mrefai.

21 Naye huyo alipowatukana Israeli, ndipo Yonathani, mwana wa Shimei, nduguye Daudi, akamwua.

22 Hao wanne walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gathi; wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mikono ya watumishi wake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo