Yakobo 5 - Swahili Revised Union VersionOnyo kwa matajiri wadhalimu 1 Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige mayowe kwa sababu ya mateso yenu yanayowajia. 2 Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. 4 Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliokosa kuwalipa kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. 5 Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejinenepesha mioyo yenu kama kwa siku ya kuchinjwa. 6 Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi. Uvumilivu katika mateso 7 Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. 8 Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. 9 Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. 10 Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. 11 Angalieni, twawaita heri wao waliostahimili. Mmesikia habari za kustahimili kwake Ayubu, kuona mwisho Bwana aliyomtendea, jinsi Bwana alivyo mwingi wa rehema na mwenye huruma. 12 Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali “ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, msije mkaanguka katika hukumu. Sala ya imani 13 Kuna mtu miongoni mwenu anayeteseka? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. 14 Mtu wa kwenu amekuwa mgonjwa? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. 15 Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. 16 Basi ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, ili mpate kuponywa. Sala yake mwenye haki ina nguvu nyingi, na hutenda mengi. 17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia sawa na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. 19 Ndugu zangu, mtu yeyote miongoni mwenu akipotoka mbali na kweli, na kurejeshwa na mtu mwingine; 20 jueni ya kuwa yeye amrejeshaye mwenye dhambi hadi akatoka katika njia ya upotevu, ataokoa roho ya mwenye dhambi kutoka mauti, na kufunika wingi wa dhambi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya