Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Walawi 8 - Swahili Revised Union Version


Kanuni za kuweka makuhani

1 BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2 Mtwae Haruni, na wanawe pamoja naye, na yale mavazi, na mafuta ya kutia, na ng'ombe dume wa sadaka ya dhambi, na kondoo wawili wa kiume, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu;

3 kisha ukutanishe mkutano wote hapo mlangoni pa hema ya kukutania.

4 Basi Musa akafanya kama alivyoambiwa na BWANA; na huo mkutano ulikutanishwa mlangoni pa hema ya kukutania.

5 Musa akawaambia mkutano, Neno aliloliagiza BWANA kwamba lifanywe, ni hili.

6 Basi Musa akawaleta Haruni na wanawe, akawaosha kwa maji.

7 Kisha akamvika Haruni ile kanzu, na kumfunga mshipi, na kumvika joho, na kumvika naivera, na kumfunga huo mshipi wa kazi ya stadi wa naivera na kumfunga naivera kwa huo mshipi.

8 Kisha akamtia kile kifuko cha kifuani; akatia hizo Urimu na Thumimu katika hicho kifuko cha kifuani.

9 Akamvika na kile kilemba kichwani mwake; na juu ya kilemba, upande wa mbele, akakitia kile kipande cha dhahabu, hilo taji takatifu; kama BWANA alivyomwagiza Musa.

10 Kisha Musa akatwaa hayo mafuta matakatifu ya kutia, akatia mafuta maskani, na vyote vilivyokuwamo, na kuvitakasa.

11 Kisha akanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kuitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na kitako chake, ili kuvitakasa.

12 Kisha akamimina mafuta hayo ya kutia kichwani mwake Haruni, na kumtia mafuta, ili amtakase.

13 Kisha Musa akawaleta wana wa Haruni, na kuwavika kanzu, na kuwafunga mishipi, na kuwavika vilemba; kama BWANA alivyomwagiza Musa.

14 Kisha akamleta yule ng'ombe dume wa sadaka ya dhambi; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao katika kichwa cha huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi.

15 Kisha akamchinja; na Musa akaitwaa damu yake, akaitia katika pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake, akaitakasa madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu, na kuitakasa, ili afanye upatanisho kwa ajili yake.

16 Kisha akayatwaa mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo yake, na kitambi kilichokuwa katika ini, na figo zake mbili, na mafuta yake, na Musa akayateketeza juu ya madhabahu.

17 Lakini huyo ng'ombe mwenyewe, na ngozi yake, na nyama yake, na mavi yake, akaviteketeza nje ya kambi; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.

18 Kisha akamsongeza yule kondoo dume wa sadaka ya kuteketezwa; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.

19 Kisha akamchinja; na Musa akainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.

20 Kisha akamkata kondoo vipande vyake; na Musa akateketeza kichwa, na vile vipande, na mafuta.

21 Kisha akayaosha matumbo na miguu yake kwa maji; na Musa akamteketeza huyo kondoo wote juu ya madhabahu; ilikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza; ilikuwa ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto; kama BWANA alivyomwagiza Musa.

22 Kisha akamsongeza kondoo dume wa pili, huyo kondoo wa kuwaweka wakfu; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.

23 Kisha akamchinja; na Musa akatwaa baadhi ya damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kulia la Haruni, na katika kidole cha gumba cha mkono wake wa kulia, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kulia.

24 Kisha akawaleta wana wa Haruni, na Musa akaitia hiyo damu katika ncha za masikio ya upande wa kulia, na katika vidole vya gumba vya mikono yao ya kulia, na katika vidole vya gumba vya maguu yao ya kulia; kisha Musa akainyunyiza hiyo damu katika madhabahu pande zote.

25 Kisha akayatwaa hayo mafuta, na mkia wenye mafuta, na mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo, na kitambi cha ini, na figo mbili, na mafuta yake, na mguu wa nyuma wa upande wa kulia;

26 kisha kutoka kwa kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichokuwa pale mbele za BWANA, akatwaa mkate mmoja usiochachwa, na mkate mmoja ulioandaliwa na mafuta na kaki moja nyembamba, akaiweka juu ya mafuta, na juu ya huo mguu wa nyuma wa upande wa kulia;

27 kisha akaweka vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe, na kuvitikisa huku na huko viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA.

28 Kisha Musa akavitwaa tena mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa vilikuwa vya kuwaweka wakfu, ni harufu nzuri; ilikuwa dhabihu iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto.

29 Kisha Musa akakitwaa kile kidari, akakitikisa huku na huko, kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; ni sehemu ya Musa katika huyo kondoo dume wa kuwaweka wakfu; kama BWANA alivyomwagiza Musa.

30 Kisha Musa akatwaa baadhi ya mafuta ya kutia, na ya damu iliyokuwa pale juu ya madhabahu, na kumnyunyizia Haruni, katika mavazi yake, na wanawe, katika mavazi yao; akamtakasa Haruni, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe waliokuwa pamoja naye.

31 Kisha Musa akawaambia huyo Haruni na wanawe, Tokoseni hiyo nyama mlangoni pa hema ya kukutania; mkaile pale pale, na hiyo mikate iliyo katika kile kikapu cha kuwaweka wakfu, kama nilivyoagizwa kusema, Haruni na wanawe wataila.

32 Nacho kitakachosalia katika hiyo nyama na mikate mtakichoma moto.

33 Wala msitoke nje mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba, hadi siku za kuwekwa wakfu kwenu zitakapotimia; kwa kuwa atawaweka muda wa siku saba.

34 Vile vile kama ilivyotendeka siku ya leo, ndivyo BWANA alivyoagiza, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.

35 Nanyi mtakaa mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba mchana na usiku, na kuulinda ulinzi wa BWANA ili kwamba msife; kwani ndivyo nilivyoagizwa.

36 Basi Haruni na wanawe wakafanya mambo hayo yote BWANA aliyoyaagiza kwa mkono wa Musa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo