Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Nehemia 13 - Swahili Revised Union Version


Wageni watengwa kutoka Israeli

1 Siku hiyo walisoma katika kitabu cha Musa masikioni mwa watu; na ndani yake yalionekana maneno haya yameandikwa, ya kwamba Mwamoni na Mmoabi wasiingie katika kusanyiko la Mungu milele;

2 kwa sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa baraka.

3 Ikawa walipoisikia Torati, wakawatenga Israeli na umati wa watu waliochanganyika nao.


Matengenezo ya Nehemia

4 Na kabla ya hayo, Eliashibu, kuhani, aliyewekwa avisimamie vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, kwa kuwa alikuwa jamaa yake Tobia,

5 alikuwa amemtengenezea chumba kikubwa, hapo walipoweka zamani sadaka za unga, na ubani, na vyombo, na zaka za nafaka, na divai, na mafuta, walivyoamriwa kuwapa Walawi, na waimbaji, na mabawabu; tena sadaka za kuinuliwa zilizokuwa za makuhani.

6 Lakini wakati huo wote mimi sikuwako huko Yerusalemu; maana katika mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta, mfalme wa Babeli, nilimrudia mfalme; na baada ya siku kadhaa nikaomba ruhusa tena kwa mfalme.

7 Nami nikaja Yerusalemu, nikafahamu yale mabaya, ambayo Eliashibu ameyatenda kwa ajili ya Tobia, kwa kumtengenezea chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.

8 Nami nikasikitika sana; basi nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia vitoke humo chumbani.

9 Kisha nikatoa amri, nao wakavisafisha vyumba; nami nikavirudisha humo vyombo vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za unga na ubani.

10 Tena nikagundua kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao; Hivyo Walawi na waimbaji walioongoza ibada, kila mtu amerudi shambani mwake.

11 Ndipo nikagombana na viongozi, nikasema, Mbona nyumba ya Mungu imeachwa? Kisha nikawakusanya, nikawaweka mahali pao.

12 Ndipo Yuda wote walipoleta zaka za nafaka, na mvinyo, na mafuta, kwenye hazina.

13 Nami nikawaweka watunza hazina juu ya hazina, yaani, Shelemia kuhani, na Sadoki mwandishi, na wa Walawi, Pedaya; na wa pili wao alikuwa Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania; kwani walihesabiwa kuwa waaminifu, na ilikuwa juu yao kuwagawia ndugu zao.

14 Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, na kwa taratibu zake.


Matengenezo ya Sabato

15 Siku hizo niliona katika Yuda watu wengine waliosindika zabibu ili kupata mvinyo siku ya sabato, na wengine waliochukua miganda, na kuwapakia punda zao; tena na mvinyo, na zabibu, na tini, na namna zote za mizigo, waliyoileta Yerusalemu, siku ya sabato; nami nikashuhudia juu yao siku ile waliyouza vyakula.

16 Tena watu wa Tiro walioleta samaki na biashara za kila namna wakakaa mumo humo, wakawauzia watu wa Yuda na Yerusalemu siku ya sabato.

17 Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato?

18 Je! Sivyo hivyo walivyofanya baba zenu; na Mungu wetu, je! Hakuyaleta mabaya haya yote juu yetu, na juu ya mji huu? Nanyi hata hivyo mnazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi sabato!

19 Ikawa malango ya Yerusalemu yalipoanza kuwa na giza kabla ya sabato, niliamuru milango ifungwe, nikaamuru isifunguliwe hata sabato iishe; na baadhi ya watumishi wangu nikawaweka juu ya malango, ili usiingizwe mzigo wowote siku ya sabato.

20 Basi wenye biashara na wachuuzi wa bidhaa za kila namna wakalala nje ya Yerusalemu mara moja au mbili.

21 Ndipo nikawashuhudia, nikawaambia, Mbona mnalala nje ya mji? Mkitenda hivi tena, nitawakamata. Tangu wakati ule hawakuja tena siku ya sabato.

22 Kisha nikawaamuru Walawi wajitakase, nao waje kuyalinda malango, ili kuitakasa siku ya sabato. Unikumbukie hayo nayo, Ee Mungu wangu, ukaniachilie sawasawa na wingi wa rehema zako.


Ndoa za mseto zapigwa marufuku

23 Tena siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na Amoni, na Moabu;

24 na nusu ya watoto wao wakazungumza kwa lugha ya Ashdodi, wala hawakuweza kuzungumza Kiyahudi, bali kwa lugha mojawapo ya watu hao.

25 Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.

26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; lakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye.

27 Basi, na sisi, je! Tuwasikilize ninyi kutenda neno hili baya, hata kumkosea Mungu wetu kwa kuwaoa wanawake wageni?

28 Na mwana mmoja wa Yoyada, mwana wa Eliashibu, kuhani mkuu, alikuwa mkwewe Sanbalati, Mhoroni, basi nikamfukuza kwangu.

29 Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, jinsi walivyounajisi ukuhani, na agano la ukuhani na la Walawi.

30 Hivyo nikawatakasa na kila kitu kigeni, nami nikawawekea zamu makuhani na Walawi, kila mtu kazini mwake;

31 na kuleta kwa kuni na malimbuko, katika nyakati zilizoamriwa. Nikumbuke, Ee Mungu wangu, ili unitendee mema.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo