Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mwanzo 15 - Swahili Revised Union Version


Agano la Mungu na Abramu

1 Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako itakuwa kubwa sana.

2 Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?

3 Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.

4 Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali utakayemzaa ndiye atakayekurithi.

5 Akamtoa nje, akasema, Tazama juu mbinguni kisha uzihesabu nyota, kama unaweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.

6 Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.

7 Kisha akamwambia, Mimi ni BWANA, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uimiliki.

8 Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitaimiliki?

9 Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo dume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa.

10 Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua.

11 Na tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza.

12 Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia.

13 BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa kwa muda wa miaka mia nne.

14 Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali nyingi.

15 Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.

16 Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana uovu wa Waamori haujatimia bado.

17 Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuri ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama.

18 Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati,

19 Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni,

20 na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai,

21 na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo