Hesabu 12 - Swahili Revised Union VersionHaruni na Miriamu wamwonea wivu Musa 1 Kisha Miriamu na Haruni wakamteta Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. 2 Wakasema, Je! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao. 3 Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. 4 BWANA akanena ghafla na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. 5 BWANA akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili. 6 Kisha akawaambia, Sikilizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. 7 Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; 8 Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumteta mtumishi wangu, huyo Musa? 9 Hasira za BWANA zikawaka juu yao; kisha akaenda zake. 10 Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na na kumwona akiwa mwenye ukoma. 11 Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. 12 Nakusihi, asiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo tumbo la mama yake. 13 Musa akamlilia BWANA, akasema, Mponye, Ee Mungu, nakusihi sana. 14 BWANA akamwambia Musa, Je! Kama baba yake angalimtemea mate usoni tu, hangaliona aibu muda wa siku saba? Na afungwe nje ya kambi muda wa siku saba, kisha baada ya hayo ataletwa ndani tena. 15 Basi Miriamu alifungwa nje ya kambi muda wa siku saba; wala watu hawakusafiri hata Miriamu alipoletwa ndani tena. 16 Baada ya hayo watu wakasafiri kutoka Haserothi, wakapiga kambi katika nyika ya Parani. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya