Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

1 Timotheo 4 - Swahili Revised Union Version


Kujinyima kusikofaa

1 Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine wataikana imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

3 wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.

4 Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani;

5 kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.


Mtumishi mwema wa Yesu Kristo

6 Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoefu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata.

7 Bali hadithi za kale, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa.

8 Maana, mazoezi ya viungo vya mwili yana manufaa kidogo, lakini utauwa una manufaa ya kila aina; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.

9 Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa;

10 kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa wale waaminio.

11 Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha.

12 Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.

13 Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma Maandiko, kuonya na kufundisha.

14 Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono na wazee.

15 Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote.

16 Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako, na wale wakusikiao pia.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo