Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

1 Samueli 28 - Swahili Revised Union Version

1 Ikawa siku zile hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao waende vitani, ili kupigana na Israeli. Naye Akishi akamwambia Daudi, Jua hakika ya kuwa wewe utatoka pamoja nami jeshini, wewe na watu wako.

2 Naye Daudi akamwambia Akishi, Vema, sasa utajua atakayoyatenda mtumishi wako. Naye Akishi akamwambia Daudi, Haya basi! Mimi nitakufanya wewe kuwa mlinzi wangu binafsi daima.


Sauli amwendea mtambuzi

3 Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi.

4 Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa.

5 Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana.

6 Lakini Sauli alipouliza kwa BWANA, BWANA hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii.

7 Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori.

8 Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye pamoja na watu wawili wakamfikia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukaniletee yeye nitakayemtaja kwako.

9 Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua?

10 Naye Sauli akamwapia kwa BWANA, akasema, Aishivyo BWANA, haitakupata adhabu yoyote kwa jambo hili.

11 Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekuletea? Naye akasema, Niletee Samweli.

12 Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli.

13 Mfalme akamwambia Usiogope; unaona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu akitoka katika nchi.

14 Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka chini, akasujudia.

15 Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje.

16 Samweli akasema, Kwa nini unaniuliza mimi, wakati BWANA amekuacha, naye amekuwa adui yako?

17 Yeye BWANA amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; BWANA amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi.

18 Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya BWANA, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii BWANA amekutendea hili leo.

19 Tena pamoja na wewe BWANA atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena BWANA atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti.

20 Mara Sauli akaanguka chini kifudifudi, akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli, wala hakuwa na nguvu yoyote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha.

21 Ndipo yule mwanamke akamwendea Sauli na alipoona kuwa yeye ametaabika sana, akamwambia, Angalia, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako, nami nimehatarisha uhai wangu, nami nimeyasikiliza maneno yako uliyoniambia.

22 Basi sasa, tafadhali, wewe uisikilize sauti ya mjakazi wako, nikakuandalie angaa mkate kidogo; ukale, ili upate nguvu, utakapokwenda zako.

23 Lakini yeye alikataa, akasema, Mimi sitaki kula. Ila watumishi wake, pamoja na yule mwanamke, wakamlazimisha; naye akaisikiliza sauti yao. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.

24 Naye yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona nyumbani; akafanya haraka kumchinja; akatwaa na unga, akaukanda, akafanya mkate wa mofa kwa unga huo;

25 kisha akamwandalia Sauli na watumishi wake; wakala. Ndipo wakaondoka, wakaenda zao usiku ule.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo