Zekaria 5 - Swahili Revised Union VersionMaono ya sita: Gombo linalopuruka 1 Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la kitabu lirukalo. 2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la kitabu lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi. 3 Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atakatiwa mbali kama ilivyoandikwa upande, na kwa hiyo kila aapaye kwa uongo atakatiliwa mbali kama ilivyo andikwa upande wa pili. 4 Nitaituma itokee, asema BWANA wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi, na katika nyumba ya yeyote aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katika nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake. Maono ya saba: Mwanamke akiwa katika kikapu 5 Ndipo yule malaika aliyesema nami akatokea, akaniambia, Inua macho yako sasa, uone ni kitu gani kitokeacho. 6 Nikasema, Ni kitu gani? Akasema, Kitu hiki ni efa itokeayo. Tena akasema, Huu ndio uovu wao katika nchi hii yote; 7 na tazama, kifuniko cha risasi kiliinuliwa; na tazama, mlikuwa na mwanamke ndani ya kikapu. 8 Akasema, Huyu ni Uovu; akamsukuma ndani ya kile kikapu; akalitupa lile jiwe la risasi juu ya mdomo wa ile efa. 9 Ndipo nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, wanawake wawili walitokea, nao upepo ulikuwa katika mabawa yao; na mabawa yao yalikuwa kama mabawa ya korongo; wakaiinua ile efa kati ya dunia na mbingu. 10 Ndipo nikamwambia yule malaika aliyesema nami, Hawa wanaipeleka wapi efa hii? 11 Akaniambia, Wanakwenda kumjengea nyumba katika nchi ya Shinari; tena ikiisha kutengenezwa, atawekwa huko mahali pake mwenyewe. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya