Waebrania 3 - Swahili Revised Union VersionMusa ni mtumishi, Kristo ni Mwana 1 Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu, 2 aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu. 3 Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba. 4 Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu. 5 Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye; 6 bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya tumaini letu mpaka mwisho. Onyo juu ya kutoamini 7 Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mkisikia sauti yake, 8 Msifanye mioyo yenu kuwa migumu, Kama wakati wa kuasi, Siku ya kujaribiwa katika jangwa, 9 Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arubaini. 10 Kwa hiyo nilichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu; 11 Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu. 12 Hadharini, ndugu zangu, usiwepo katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutoamini, ujitengao na Mungu aliye hai. 13 Lakini mwonyane kila siku, maadamu inaitwa leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. 14 Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho; 15 kama inenwavyo, Leo, kama mkisikia sauti yake, Msifanye mioyo yenu kuwa migumu, Kama wakati wa kuasi. 16 Maana ni akina nani walioasi, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa? 17 Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arubaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa? 18 Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika pumziko lake, ila wale walioasi? 19 Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutoamini kwao. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya