Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Waebrania 2 - Swahili Revised Union Version


Onyo kuhusu kuwa makini

1 Kwa hiyo imetupasa kuyaangalia zaidi hayo tuliyoyasikia tusije tukayakosa.

2 Kwa maana, ikiwa lile neno lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki,

3 sisi je! Tutapataje kupona, tukipuuza wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliomsikia;

4 Mungu naye akishuhudia pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa karama za Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe.


Kutukuka kwa kujishusha

5 Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema,

6 Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie?

7 Umemfanya mdogo kwa muda kuliko malaika, Umemvika taji la utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;

8 Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakubakiza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hamjaona vitu vyote kutiwa chini yake,

9 ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo kwa muda kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji la utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.

10 Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.

11 Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake;

12 akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa.

13 Na tena, Nitakuwa nimemtumaini yeye. Na tena, Tazama, mimi nipo hapa na watoto niliopewa na Mungu.

14 Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,

15 awaache huru wale ambao katika maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.

16 Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Abrahamu.

17 Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye kafara ya suluhu kwa dhambi za watu wake.

18 Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo