Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Ufunuo 5 - Swahili Revised Union Version


Kitabu na Mwana-kondoo

1 Kisha nikaona katika mkono wa kulia wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa mihuri saba.

2 Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, Ni nani anayestahili kukifungua kitabu, na kuivunja mihuri yake?

3 Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua kitabu hicho, wala kukitazama.

4 Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua kitabu hicho, wala kukitazama.

5 Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila la Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na ile mihuri yake saba.

6 Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote.

7 Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kulia wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi.

8 Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.

9 Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuifungua mihuri yake; kwa kuwa ulichinjwa, ukawa fidia kwa Mungu na kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,

10 ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

11 Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa maelfu na mamilioni,

12 wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.

13 Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi na juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nilivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na kwake Mwana-kondoo, hata milele na milele.

14 Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo