Nahumu 2 - Swahili Revised Union VersionMaangamizi ya mji mwovu 1 Yeye apondaye vipande vipande amepanda juu mbele ya uso wako; zishike silaha, ilinde njia, vitie nguvu viuno vyako, uongeze uwezo wako sana. 2 Kwa maana BWANA anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao. 3 Ngao ya mashujaa wake imefanywa kuwa nyekundu, watu walio hodari wa vita wamevaa nguo nyekundu sana; magari ya vita yametameta kwa chuma cha pua siku ya kukusanywa kwake, na mikuki inatikiswa kwa namna ya kutisha. 4 Magari ya vita yanafanya vishindo njiani, Yanasonganasongana katika njia kuu; Kuonekana kwake ni kama mienge, Yanakwenda upesi kama umeme. 5 Awakumbuka watu wake wenye heshima; Wanajikwaa katika mwendo wao; Wanafanya haraka waende ukutani; Nacho kitu cha kuwafunika kimetayarishwa. 6 Malango ya mito yamefunguka, na jumba la mfalme limeyeyushwa. 7 Husabu naye amefunuliwa, anachukuliwa, na wajakazi wake wanalia kama kwa sauti ya hua, wakipigapiga vifua vyao. 8 Lakini Ninawi tokea zamani amekuwa kama ziwa la maji; ila hata sasa wanakimbia; Simameni! Simameni! Lakini hapana hata mmoja atazamaye nyuma. 9 Chukueni nyara za fedha; Chukueni nyara za dhahabu; Kwa maana ni akiba isiyoisha, Fahari ya vyombo vipendezavyo. 10 Amekuwa utupu, na ukiwa, na uharibifu; hata moyo unayeyuka, na magoti yanagonganagongana; moyoni kote mna uchungu, na nyuso za wote zimekuwa nyeupe kwa hofu. 11 Kao la simba li wapi? Na mahali walishapo wanasimba pa wapi, mahali walipotembea simba mume na simba mke na mwanasimba, wala hapana aliyewatia hofu? 12 Simba alirarua vipande vipande chakula cha kuwatosha watoto wake, aliwakamatia majike wake mawindo, aliyajaza mapango yake mateka, na makao yake aliyajaza nyama iliyoraruliwa. 13 Tazama, mimi ni juu yako, asema BWANA wa majeshi, nami nitayateketeza magari yako ya vita katika moshi, na upanga utawaangamiza wanasimba wako; nami nitayakatilia mbali mawindo yako katika nchi, na sauti za wajumbe wako hazitasikiwa tena kamwe. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya