Mhubiri 4 - Swahili Revised Union Version1 Kisha nikarudi na kuona udhalimu wote unaotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, lakini wale walikuwa hawana mfariji. 2 Kwa hiyo nikawasifu wafu waliokwisha kufa kuliko wenye uhai walio hai bado; 3 naam, zaidi ya hao wote nikamwita heri yeye asiyekuwako bado, ambaye hakuyaona mabaya yanayotendeka chini ya jua. 4 Tena nikagundua kuwa juhudi zote, na ustadi wote katika kazi, hutokana na mtu kumwonea mwingine wivu. Hayo nayo ni ubatili na kufukuza upepo. 5 Mpumbavu huikunja mikono yake, Naye hula chakula chake mwenyewe; 6 Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kufukuza upepo. 7 Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua. 8 Kuna mtu aliye peke yake, wala hana mwenzi wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema? Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa. Thamani ya kuwa na rafiki 9 Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Kwa sababu wana tuzo njema kwa kazi yao. 10 Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! 11 Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kupata moto? 12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watamstahimili; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi. 13 Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo. 14 Kwa maana anaweza kutoka gerezani kutawala; hata ikiwa alizaliwa akiwa maskini katika ufalme. 15 Nikawaona wote walio hai waendao chini ya jua, ya kwamba walishikamana na huyo kijana, huyo wa pili aliyesimama badala ya mfalme. 16 Hawakuwa na kikomo hao watu wote, hao wote ambao alikuwa juu yao; lakini hata hivyo wale wafuatao baada yake hawatamfurahia. Hakika hayo pia ni ubatili, na kufukuza upepo. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya