Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hosea 6 - Swahili Revised Union Version


Mwito wa toba

1 Njooni, tumrudie BWANA; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga majeraha yetu.

2 Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.

3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua BWANA; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.


Uovu wa Israeli na Yuda

4 Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.

5 Kwa sababu hiyo nimewakatakata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga.

6 Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.

7 Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana.

8 Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu.

9 Na kama vile makundi ya wanyang'anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana.

10 Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi.

11 Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo