Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hagai 1 - Swahili Revised Union Version


Agizo la kulijenga hekalu tena

1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake nabii Hagai, kusema,

2 BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Wakati wa kuijenga upya nyumba ya BWANA haujafika.

3 Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

4 Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?

5 Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.

6 Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamtosheki na vinywaji; mnajivika nguo lakini hampati joto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotobokatoboka.

7 BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.

8 Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema BWANA.

9 Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha mbali. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu yumba yangu imebaki kuwa gofu la nyumba, wakati ambapo kila mmoja wenu anakimbilia nyumbani kwake.

10 Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake.

11 Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono.

12 Ndipo Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, pamoja na hao watu wote waliokuwa wamebaki, wakaitii sauti ya BWANA, Mungu wao, na maneno ya nabii Hagai, kama BWANA, Mungu wao, alivyomtuma; nao watu wakaogopa mbele za BWANA.

13 Ndipo Hagai mjumbe wa BWANA, katika ujumbe wa BWANA, akawaambia watu ujumbe wa BWANA, akisema, Mimi nipo pamoja nanyi, asema BWANA.

14 BWANA akaiamsha roho ya Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na roho ya Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na roho za watu waliokuwa wamebaki; wakaenda, wakafanya kazi katika nyumba ya BWANA wa majeshi, Mungu wao;

15 katika siku ya ishirini na nne ya mwezi, katika mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa mfalme Dario.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo