1 Samueli 11 - Swahili Revised Union VersionSauli awashinda Waamoni 1 Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni, akakwea na kupiga kambi juu ya Yabesh-gileadi; na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi, na sisi tutakutumikia. 2 Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hili mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kulia; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia. 3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende kote mipakani mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutajisalimisha kwako. 4 Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia. 5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi. 6 Na Roho ya Mungu ikamjia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana. 7 Akachukua fahali wawili waliofungwa nira, akawakatakata vipande, kisha akawatuma wajumbe kuvipeleka vile vipande kote katika Israeli, wakisema, Yeyote ambaye hatamfuata Sauli na Samweli, ng'ombe wake watafanyiwa vivi hivi. Basi utisho wa BWANA ukawaangukia wale watu, wakatoka kwa pamoja. 8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa elfu mia tatu, na Wayuda elfu thelathini. 9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao wakafurahi. 10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema. 11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya kambi kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hadi wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja. 12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue. 13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo BWANA amefanya wokovu katika Israeli. 14 Kisha Samweli akawaambia watu, Haya! Na twendeni mpaka Gilgali, ili tuuanzishe ufalme upya huko. 15 Nao watu wote wakaenda Gilgali; wakamtawaza Sauli mbele za BWANA huko Gilgali; wakachinja sadaka za amani mbele za BWANA; na huko Sauli na watu wote wa Israeli wakafurahi sana. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya