Yoshua 14 - Swahili Revised Union VersionMgawanyo wa nchi ya magharibi mwa Yordani 1 Kisha hizi ndizo nchi ambazo wana wa Israeli walizitwaa katika nchi ya Kanaani, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na vichwa vya nyumba za mababa wa makabila ya Israeli, waliwagawanyia, 2 kwa kufuata hiyo kura ya urithi wao, vile vile kama BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa, kwa ajili ya hayo makabila tisa, na hiyo nusu ya kabila. 3 Kwa kuwa Musa alikuwa amekwisha kuwapa urithi hayo makabila mawili na nusu, ng'ambo ya pili ya Yordani; lakini hakuwapa Walawi urithi wowote kati yao. 4 Kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa makabila mawili, Manase na Efraimu; nao hawakuwapa Walawi sehemu katika hiyo nchi, isipokuwa waliwapa miji wapate kuikaa, pamoja na viunga vyake kwa ajili ya mifugo wao, na kwa ajili ya riziki zao. 5 Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya hivyo, nao wakaigawanya hiyo nchi. Kalebu Agawiwa Hebroni 6 Wakati huo wana wa Yuda walimwendea Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno BWANA alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea. 7 Mimi nilikuwa mtu wa miaka arubaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa BWANA aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. 8 Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo; ila mimi nilimfuata BWANA, Mungu wangu, kwa utimilifu. 9 Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata BWANA, Mungu wako, kwa utimilifu. 10 Sasa basi, angalia, yeye BWANA ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arubaini na mitano, tangu wakati huo BWANA alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli walipokuwa wanapitia jangwani; na sasa tazama, hivi leo nimetimiza umri wa miaka themanini na mitano. 11 Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kwenda na kurudi. 12 Basi sasa unipe mlima huu, ambao BWANA alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye BWANA atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama BWANA alivyonena. 13 Yoshua akambariki, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake. 14 Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi hata hivi leo, kwa sababu, alikuwa mwaminifu kwa BWANA, Mungu wa Israeli. 15 Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya