Yona 2 - Swahili Revised Union VersionWimbo wa kushukuru 1 Ndipo Yona akamwomba BWANA, Mungu wake, akiwa katika tumbo la yule samaki, 2 Akasema, Nilimlilia BWANA kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu niliomba, Nawe ukasikia sauti yangu. 3 Maana ulinitupa vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu. 4 Nami nikasema, Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu. 5 Maji yalinizunguka, hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu; 6 Nilishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi ambayo mapingo yake yanafunga hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka humo shimoni, Ee BWANA, Mungu wangu, 7 Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nilimkumbuka BWANA; Maombi yangu yakakufikia, Katika hekalu lako takatifu. 8 Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo Hujitenga na rehema zao wenyewe. 9 Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu. Wokovu hutoka kwa BWANA. 10 BWANA akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona katika pwani. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya