Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Nehemia 6 - Swahili Revised Union Version


Kushindwa kwa adui

1 Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakubakia mapengo ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);

2 Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Lakini wakakusudia kunifanyia mabaya.

3 Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, siwezi kushuka, kwa nini niwashukie na hapo kazi isimame?

4 Nao wakaniletea mwito huo mara nne; nikawajibu maneno yale yale.

5 Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumishi wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;

6 nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mnakusudia kuasi; ndiyo sababu unaujenga huo ukuta; nawe unataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.

7 Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu kwa kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa mfalme ataarifiwa mambo haya, Basi sasa, njoo ili tushauriane.

8 Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni.

9 Kwani hao wote walitaka kutuogofya, wakisema, Kwa kuwa mikono yao italegea katika kazi, kazi isifanyike. Lakini sasa Ee Mungu, itie nguvu mikono yangu.

10 Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa kifungo cha nyumbani; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, na tuifunge milango ya hekalu; kwa kuwa watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua.

11 Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.

12 Nikatambua, na tazama, si Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; kwa kuwa Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.

13 Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.

14 Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, Tobia na Sanbalati kulingana na hayo matendo yao, na yule nabii mwanamke Noadia.


Ukuta wakamilika

15 Basi huo ukuta ukakamilika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili.

16 Ikawa adui zetu wote waliposikia, ndipo wamataifa wote waliotuzunguka wakaogopa, nao wakakata tamaa sana machoni pao wenyewe; maana waliitambua kazi hiyo ilivyotendwa na Mungu wetu.

17 Tena siku zile wakuu wa Yuda walimtumia nyaraka nyingi Tobia nazo nyaraka za Tobia ziliwafikia.

18 Kwa maana walikuwa watu wengi katika Yuda waliomwapia, kwa sababu alikuwa mkwewe Shekania, mwana wa Ara; naye Yehohanani mwanawe amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.

19 Tena waliyanena mema yake mbele yangu, na kumwambia maneno yangu. Tobia naye akaniletea mimi nyaraka za kuniogofya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo