Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Matendo 23 - Swahili Revised Union Version

1 Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi.

2 Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake.

3 Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu kulingana na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

4 Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu?

5 Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako.

6 Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.

7 Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana.

8 Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote.

9 Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wowote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini?

10 Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akahofia Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome.

11 Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.


Njama za kumwua Paulo

12 Kulipopambazuka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hadi wamwue Paulo.

13 Na hao walioapiana hivyo walikuwa zaidi ya watu arubaini.

14 Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo.

15 Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tuko tayari kumwua kabla hajakaribia.

16 Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari.

17 Paulo akamwita ofisa mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu.

18 Basi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia.

19 Yule jemadari akamshika mkono akajitenga pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu?

20 Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi.

21 Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arubaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hadi watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakisubiri kusikia utasemaje.

22 Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniambia haya.


Paulo atumwa kwa Feliki mtawala

23 Akawaita maofisa wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kabla ya saa tatu usiku.

24 Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki mtawala.

25 Akaandika barua, juu ya hili,

26 Klaudio Lisia kwa mtawala mtukufu Feliki, Salamu!

27 Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi, wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni Mrumi.

28 Nami nikitaka kulijua lile neno walilomshitakia, nikamteremsha nikamweka mbele ya baraza;

29 nikaona kwamba ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lolote la kustahili kuuawa wala kufungwa.

30 Hata nilipopewa habari kwamba patakuwa na ghasia juu ya mtu huyu, mara nikamtuma kwako, nikawaagiza na wale waliomshitaki, wanene habari zake mbele yako. Wasalamu.

31 Basi, wale askari wakamchukua Paulo kama walivyoamriwa, wakampeleka hadi Antipatri usiku;

32 hata asubuhi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi zao ngomeni.

33 Na wale walipofika Kaisaria, na kumpa mtawala ile barua, wakamweka Paulo mbele yake.

34 Naye alipokwisha kuisoma, akawauliza, Mtu huyu ni wa mkoa gani? Alipoarifiwa ya kuwa ni mtu wa Kilikia,

35 akasema, Nitakusikia wewe watakapokuja wale waliokushitaki; akaamuru alindwe katika nyumba ya utawala wa Herode.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo