Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hesabu 34 - Swahili Revised Union Version


Mipaka ya nchi

1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2 Waagize wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapoingia nchi ya Kanaani, (hii ndiyo nchi itakayowaangukia kuwa urithi, maana, hiyo nchi ya Kanaani kama mipaka yake ilivyo,)

3 ndipo upande wenu wa kusini utakuwa tangu bara ya Sini kupita kando ya Edomu, na mpaka wenu wa kusini utakuwa tangu mwisho wa Bahari ya Chumvi kuelekea mashariki;

4 kisha mpaka wenu utageuka kwenda upande wa kusini wa kukwelea kwake Akrabimu, kisha kupita kwendelea Sini; na kutokea kwake kutakuwa kuelekea upande wa kusini wa Kadesh-barnea; kisha utaendelea mpaka Hasar-adari, na kufikia Azmoni;

5 kisha mpaka utageuka kutoka Azmoni kwendelea kijito cha Misri, na kutokea kwake kutakuwa hapo baharini.

6 Kisha mpaka wenu wa upande wa magharibi mtakuwa na bahari kubwa na mpaka wake; huu ndio mpaka wenu upande wa magharibi.

7 Kisha mpaka wenu wa upande wa kaskazini utakuwa ni huu; kutoka bahari kubwa mtajiandikia mlima wa Hori;

8 na kutoka mlima wa Hori mtaweka alama hadi Hamathi; na kutokea kwake mpaka hadi hapo Sedada;

9 tena mpaka utatokea hadi Zifroni, na kutokea kwake kutakuwa hapo Hasarenani; huo ndio mpaka wenu wa upande wa kaskazini.

10 Kisha mtaweka mpaka wenu wa upande wa mashariki kutoka Hasarenani hadi Shefamu mpaka Ribla;

11 kisha mpaka utateremka kutoka Shefamu mpaka Ribla, upande wa mashariki wa Aini; kisha mpaka utateremka na kufikia upande wa bahari ya Kinerethi upande wa mashariki;

12 kisha mpaka utateremkia Yordani, na kutokea kwake kutakuwa hapo katika Bahari ya Chumvi; hii ndiyo nchi yenu kama mipaka yake ilivyo kuizunguka pande zote.

13 Kisha Musa akawaagiza wana wa Israeli, akisema, Hii ndiyo nchi mtakayoirithi kwa kupiga kura, ambayo BWANA ameagiza wapewe watu wa yale makabila tisa, na nusu ya kabila;

14 kwa kuwa kabila la wana wa Reubeni kwa nyumba za baba zao, na kabila la wana wa Gadi kwa nyumba za baba zao, wamekwisha pata, na hiyo nusu ya kabila la Manase wamekwisha pata urithi wao;

15 hayo makabila mawili na nusu ya kabila wamekwisha pata urithi wao huko ng'ambo ya pili ya Yordani, hapo Yeriko, upande wa mashariki, kuelekea maawio ya jua.


Viongozi wa makabila

16 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

17 Haya ndiyo majina ya watu watakaowagawanyia nchi iwe urithi wenu; Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni.

18 Kisha mtamtwaa mkuu mmoja wa kila kabila, ili waigawanye nchi iwe urithi wenu.

19 Na majina ya watu hao ni haya; katika kabila la Yuda, ni Kalebu mwana wa Yefune.

20 Na katika kabila la wana wa Simeoni, Shemueli mwana wa Amihudi.

21 Katika kabila la Benyamini, ni Elidadi mwana wa Kisloni.

22 Na katika kabila la wana wa Dani, mkuu, Buki mwana wa Yogli.

23 Katika wana wa Yusufu; katika kabila la wana wa Manase, mkuu, Hanieli mwana wa Efodi;

24 na katika kabila la wana wa Efraimu, mkuu, Kemueli mwana wa Shiftani.

25 Na katika kabila la wana wa Zabuloni, mkuu, Elisafani mwana wa Parnaki.

26 Na katika kabila la wana wa Isakari, mkuu, Paltieli mwana wa Azani.

27 Na katika kabila la wana wa Asheri, mkuu, Ahihudi mwana wa Shelomi.

28 Na katika kabila la wana wa Naftali, mkuu, Pedaheli mwana wa Amihudi.

29 Hao ndio BWANA aliowaagiza wawagawanyie urithi wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo