Hesabu 30 - Swahili Revised Union VersionNadhiri zilizofanywa na wanawake 1 Kisha Musa akanena na wale vichwa vya makabila ya wana wa Israeli, na kuwaambia, Neno hili ndilo aliloliagiza BWANA. 2 Mtu atakapomwekea BWANA nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa ahadi, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake. 3 Tena mwanamke atakapomwekea BWANA nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aishi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake; 4 babaye naye akasikia nadhiri yake, na kile kifungo chake alichofungia nafsi yake, na babaye akamnyamazia; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichofungia nafsi yake kitathibitika. 5 Lakini kama huyo babaye akimkataza siku hiyo aliyosikia; nadhiri zake ziwazo zote, wala vifungo vyake alivyoifungia nafsi yake havitathibitika; na BWANA atamsamehe, kwa kuwa babaye alimkataza. 6 Tena kama amekwisha kuolewa na mume, wakati huo wa nadhiri zake, au wa neno hilo alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; 7 na mumewe akasikia, naye akamnyamazia siku hiyo aliyosikia neno hilo; ndipo nadhiri zake zitathibitika, na vile vifungo ambavyo ameifunga nafsi yake vitathibitika. 8 Lakini kama mumewe akimkataza siku hiyo aliyolisikia; ndipo ataitangua nadhiri yake iliyo juu yake na neno alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; na BWANA atamsamehe 9 Lakini nadhiri ya mjane, au ya mwanamke aliyetalikiwa, kila neno ambalo ameifunga nafsi yake kwalo, litathibitika juu yake. 10 Tena kama aliweka nadhiri nyumbani mwa mumewe, au kama aliifunga nafsi yake kwa kifungo pamoja na kiapo, 11 na mumewe alisikia akamnyamazia, wala hakumkataza; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichojifungia kitathibitika. 12 Lakini kama mumewe alizibatilisha na kuzitangua siku hiyo aliyozisikia, ndipo kila neno lililotoka midomoni mwake katika hizo nadhiri zake, au katika kile kifungo cha nafsi yake, halitathibitika; huyo mumewe amezitangua; na BWANA atamsamehe. 13 Kila nadhiri, na kila kiapo kifungacho, ili kuitaabisha nafsi ya mwanamke mumewe aweza kuthibitisha, au mumewe aweza kutangua. 14 Lakini mumewe akimnyamazia mkewe kabisa siku hata siku ndipo azithibitisha nadhiri zote za mkewe, au vifungo vyake vyote vilivyo juu yake; yeye amezithibitisha, kwa kuwa alimnyamazia mkewe siku hiyo aliyozisikia nadhiri zake. 15 Lakini akizibatilisha na kuzitangua baada ya kuzisikia; ndipo yeye atachukua uovu wa mkewe. 16 Hizi ndizo amri, ambazo BWANA alimwagiza Musa, kati ya mtu mume na mkewe, kati ya baba na binti yake, katika ujana wake, akiwa nyumbani mwa babaye. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya