Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hagai 2 - Swahili Revised Union Version


Utukufu wa hekalu ujao

1 Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

2 Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hao watu waliokuwa wamebaki, ukisema,

3 Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?

4 Lakini sasa uwe jasiri, Ee Zerubabeli, asema BWANA; nawe uwe jasiri, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni jasiri, enyi watu wote wa nchi hii, asema BWANA; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema BWANA wa majeshi;

5 kama ilivyo ahadi niliyowawekea mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope.

6 Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Kwa mara nyingine, kitambo kidogo tu, nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu;

7 nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema BWANA wa majeshi.

8 Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi.

9 Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi.


Karipio na ahadi

10 Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

11 BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani kuhusu sheria, mkisema,

12 Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye kwa upindo wake akagusa mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula chochote, je, Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La.

13 Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je, Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi.

14 Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema BWANA; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi.

15 Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla jiwe halijatiwa juu ya jiwe katika nyumba ya BWANA;

16 katika wakati huo wote, mtu alipofikia rundo la vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia pipa kubwa apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu.

17 Niliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.

18 Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la BWANA tafakarini haya.

19 Je, Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki.


Ahadi ya Mungu kwa Zerubabeli

20 Kisha neno la BWANA likamjia Hagai mara ya pili, siku ya ishirini na nne ya mwezi, kusema,

21 Sema na Zerubabeli, mtawala wa Yuda, ukisema, Nitazitikisa mbingu na dunia;

22 nami nitakipindua kiti cha enzi cha falme, nami nitaziharibu nguvu za falme za mataifa; nami nitayapindua magari, na hao wapandao ndani yake; farasi na hao wawapandao wataanguka chini; kila mtu kwa upanga wa ndugu yake.

23 Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitakutwaa wewe, Ee Zerubabeli, mtumishi wangu, mwana wa Shealtieli, asema BWANA, nami nitakufanya kuwa kama pete yenye mhuri; kwa kuwa nimekuchagua, asema BWANA wa majeshi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo