Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Amosi 9 - Swahili Revised Union Version


Kuangamizwa kwa Israeli

1 Nilimwona Bwana akisimama karibu na madhabahu; akasema, Vipige vichwa vya nguzo, hata vizingiti vitikisike; vivunje vipande vipande juu ya kichwa cha kila mmoja wao; nami nitamwua mtu wa mwisho wao kwa upanga; hapana hata mmoja wao atakayekimbia, wala hataokoka hata mmoja wao.

2 Wajapochimba waingie katika kuzimu, mkono wangu utawatoa huko; nao wajapopanda hata mbinguni, nitawateremsha toka huko.

3 Nao wajapojificha katika kilele cha Karmeli, nitawatafuta na kuwatoa toka huko; na wajapositirika katika vilindi vya bahari nisiwaone, nitamwagiza joka huko, naye atawauma.

4 Nao wajapokwenda kuwa mateka mbele ya adui zao, nitauagiza upanga huko, nao utawaua; nami nitawaelekezea macho yangu niwatende mabaya, wala si mema.

5 Kwa maana Bwana, MUNGU wa majeshi, ndiye aigusaye nchi, nayo ikayeyuka, na wote wakaao ndani yake wataomboleza; nayo itainuka yote pia kama Nili, nayo itakupwa tena kama Mto wa Misri.

6 Yeye ndiye avijengaye vyumba vyake mbinguni, na kuweka misingi ya kuba yake juu ya nchi; yeye ndiye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA ndilo jina lake.

7 Je! Ninyi si kama wana wa Wakushi kwangu mimi, enyi wana wa Israeli, asema BWANA? Je! Mimi sikuwapandisha Israeli toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Kaftori, na Washami toka Kiri?

8 Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema BWANA.

9 Kwa maana, angalieni, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli katika mataifa yote, kama vile ngano ipepetwavyo katika ungo lakini hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini.

10 Wenye dhambi wote katika watu wangu watakufa kwa upanga, hao wasemao, Mabaya hayatatupata nyuma wala mbele.


Kurudishwa kwa ufalme wa Daudi

11 Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale;

12 wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema BWANA, afanyaye hayo.

13 Angalieni, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo huyo alimaye atamfikia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka.

14 Nami nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watatengeneza bustani, na kula matunda yake.

15 Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema BWANA, Mungu wako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo