Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

1 Samueli 7 - Swahili Revised Union Version

1 Na hao watu wa Kiriath-yearimu wakaja, wakalichukua sanduku la BWANA, wakalipeleka ndani ya nyumba ya Abinadabu huko kilimani, nao wakamtenga Eleazari, mwanawe, ili alilinde sanduku la BWANA.

2 Ikawa, tangu sanduku lipelekwe Kiriath-yearimu, muda mrefu ulipita; maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Waisraeli wakamwombolezea BWANA.


Samweli anakuwa Mwamuzi

3 Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamwelekezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti.

4 Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake.

5 Samweli akasema, Wakusanyeni Waisraeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa BWANA.

6 Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za BWANA; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia BWANA dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa.

7 Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, wakuu wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti.

8 Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia BWANA, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti.

9 Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia BWANA kwa ajili ya Israeli; BWANA akamwitikia.

10 Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; lakini BWANA akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli.

11 Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hadi walipofika chini ya Beth-kari.

12 Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Ebenezeri, akisema, Hata sasa BWANA ametusaidia.

13 Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli.

14 Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori.

15 Naye huyo Samweli akawaamua Waisraeli siku zote za maisha yake.

16 Naye huenda mwaka kwa mwaka kuzunguka mpaka Betheli, na Gilgali, na Mispa; akawaamua katika miji yote ya Israeli.

17 Kisha alikuwa akirudi Rama; maana ndipo ilipokuwa nyumba yake; nako ndiko alikowaamua Waisraeli; na huko akamjengea BWANA madhabahu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo