1 Samueli 13 - Swahili Revised Union VersionSadaka ya Sauli isiyo halali 1 Sauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha hapo alipoanza kutawala; naye akatawala miaka kadha wa kadha juu ya Israeli. 2 Naye Sauli alijichagulia watu elfu tatu wa Israeli; ambao katika hao, elfu mbili walikuwa pamoja na Sauli katika Mikmashi, na katika mlima wa Betheli na elfu moja pamoja na Yonathani katika Gibea ya Benyamini; nao wale watu waliosalia akawaruhusu waende kila mtu hemani kwake. 3 Yonathani akaipiga hiyo ngome ya Wafilisti, iliyokuwako huko Gibea, nao Wafilisti wakapata habari. Naye Sauli akapiga tarumbeta katika nchi yote, huku akisema, Na wasikie Waebrania. 4 Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali. 5 Nao Wafilisti wakakusanyika ili wapigane na Waisraeli, magari elfu thelathini, na wapanda farasi elfu sita, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni. 6 Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wako katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika. 7 Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa angali huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka. 8 Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muda uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye. 9 Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. 10 Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. 11 Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu niliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi; 12 basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za BWANA; kwa hiyo nilijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa. 13 Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya BWANA, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana BWANA angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. 14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru. Maandalizi ya vita 15 Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wakawa kama mia sita. 16 Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi. 17 Nao watekaji wa nyara wakatoka katika kambi ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali; 18 na kikosi kingine kikageukia njia iendayo Beth-horoni; na kikosi kingine kikageukia njia ya mpakani ielekeayo bonde la Seboimu upande wa nyika. 19 Basi, hakukuwa mhunzi yeyote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajitengenezea panga au mikuki; 20 lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake; 21 Na walilipa theluthi mbili za shekeli kunoa jembe na miundu, na theluthi moja ya shekeli kunoa mashoka na kuchonga michokoo. 22 Hivyo ikawa, siku ya vita, haukuonekana mkononi mwa mtu yeyote, miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani, upanga wala mkuki; isipokuwa Sauli mwenyewe na mwanawe Yonathani walikuwa navyo. Yonathani awashtua na kuwatimua Wafilisti 23 Na jeshi la Wafilisti wakatoka hata mpito ya Mikmashi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya