Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu.
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika.
Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa kwenu moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii.
‘Msiyanganganie mambo yaliyopita, wala msifikirie vitu vya zamani. Tazameni, mimi ninafanya kitu kipya. Kinafanyika sasa hivi, nanyi mtaweza kukiona. Nitafanya njia nyikani, na kububujisha mito jangwani.
Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa zake danganyifu. Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu.
alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji.
Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku.
Ndiye anayeniridhisha mema maisha yangu yote, hata nabaki kijana mwenye nguvu kama tai.
Bwana Mwenyezi-Mungu amenijaza roho yake, maana Mwenyezi-Mungu ameniweka wakfu, akanituma niwaletee wanaokandamizwa habari njema, niwatibu waliovunjika moyo, niwatangazie mateka kwamba watapata uhuru, na wafungwa kwamba watafunguliwa. Nitafurahi sana kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, nafsi yangu itashangilia kwa sababu ya Mungu wangu. Maana amenivika vazi la wokovu, amenivalisha vazi la uadilifu, kama bwana arusi ajipambavyo kwa shada la maua, kama bibi arusi ajipambavyo kwa johari zake. Hivyo, kama vile ardhi ioteshavyo mimea, na shamba lichipushavyo mbegu zilizopandwa humo, Mwenyezi-Mungu atasababisha uadilifu na sifa kuchomoza mbele ya mataifa yote. Amenituma niutangaze mwaka wake wa neema, na siku ya Mungu wetu ya kulipiza kisasi; niwafariji wote wanaoomboleza; niwape wale wanaoomboleza katika Siyoni taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya moyo mzito. Nao wataitwa mialoni madhubuti, aliyopanda Mwenyezi-Mungu kuonesha utukufu wake.
Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa tena hataweza kuuona ufalme wa Mungu.”
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Alinifundisha wimbo mpya, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu.
Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa kutokana na dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.
mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu.
Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya.
Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Ametujalia tumaini lenye uhai,
Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye.
Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.
Hivi ndivyo asemavyo Mungu aliye juu kabisa, aishiye milele na ambaye jina lake ni “Mtakatifu”: “Mimi nakaa huko juu, mahali patakatifu, nakaa pia na wenye majuto na wanyenyekevu. Mimi nitawatia moyo walio wanyenyekevu na kuwapa nguvu wenye majuto.
kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe.
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu, unipime, uyajue mawazo yangu. Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya, uniongoze katika njia ya milele.
Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu,
Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda; waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali; kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.
Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.
Mungu mwenyewe anayetupatia amani awatakase nyinyi kabisa kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu – roho, mioyo na miili yenu – mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita nyinyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.
Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.”
Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.
Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote.
Mungu amemfufua katika wafu Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele. Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.
Lakini akaniambia: “Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu.” Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu.
Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
Unifundishe kutimiza matakwa yako, maana wewe ni Mungu wangu! Roho yako nzuri iniongoze katika njia sawa.
Imarisheni mikono yenu dhaifu, kazeni magoti yenu manyonge. Waambieni waliokufa moyo: “Jipeni moyo, msiogope! Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi, atakuja kuwaadhibu maadui zenu; atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.”
Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mkombozi wangu; Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu.
Basi, nasema hivi: Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe.
Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti, huwapa hekima wasio na makuu.
Zamani nyinyi mlikuwa gizani, lakini sasa nyinyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga,
Maadamu nyinyi mmemkubali Kristo Yesu aliye Bwana, basi, ishini katika muungano naye. Muwe na mizizi ndani yake, mjijenge juu yake na kuwa imara katika imani kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele.
Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele.
Bali, shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu na matakwa yake, na hayo yote mtapewa kwa ziada.
Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema: “Mkinirudia na kutulia mtaokolewa; kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.” Lakini nyinyi hamkutaka.
Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga?
Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. “Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami nikiwa ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote.
Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo.
Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Ee Mungu, wewe u Mungu wangu, nami nakutafuta kwa moyo; roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu; nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji.
Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu.
Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu.
Nihurumie, Ee Mungu, kadiri ya fadhili zako; ufutilie mbali makosa yangu, kadiri ya wingi wa huruma yako. Uniumbie moyo safi, ee Mungu, uweke ndani yangu roho mpya na thabiti. Usinitupe mbali nawe; usiniondolee roho yako takatifu. Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa, utegemeze ndani yangu moyo wa utii. Hapo nitawafunza wakosefu njia yako, nao wenye dhambi watarudi kwako. Uniokoe na hatia ya umwagaji damu, ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, nami nitaimba kwa sauti kuwa umeniokoa. Uniwezeshe kusema, ee Bwana, midomo yangu itangaze sifa zako. Kwa kweli wewe hupendezwi na tambiko, ama sivyo mimi ningalikutolea. Wewe huna haja na tambiko za kuteketezwa. tambiko yangu kwako ee Mungu, ni moyo mnyofu; wewe, ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu. Ee Mungu, upende kuutendea mema mji wa Siyoni; uzijenge tena upya kuta za mji wa Yerusalemu. Hapo utapendezwa na tambiko za kweli: Sadaka za kuteketezwa na za kuteketezwa nzima; mafahali watatolewa tambiko madhabahuni pako. Unioshe kabisa hatia yangu; unisafishe dhambi yangu.
Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana, mwombeni msaada wakati yupo bado karibu. Waovu na waache njia zao mbaya, watu wabaya waachane na mawazo yao mabaya; wamrudie Mwenyezi-Mungu apate kuwahurumia, wamwendee Mungu wetu maana atawasamehe.
Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili.
Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu.
Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele.
Lakini nyinyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.
Pitieni milango ya hekalu lake kwa shukrani, ingieni katika nyua zake kwa sifa. Mshukuruni na kulisifu jina lake. Mwenyezi-Mungu ni mwema; fadhili zake zadumu milele, na uaminifu wake katika vizazi vyote.
Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake, mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu ni sawa na nguvu ile kuu mno
Mungu ambaye alisema, “Mwanga na uangaze kutoka gizani,” ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo.
Inuka ee Siyoni uangaze; maana mwanga unachomoza kwa ajili yako, utukufu wa Mwenyezi-Mungu unakuangaza.
Ee Mwenyezi-Mungu, ni wewe ambaye kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu, umeziumba mbingu na dunia; hakuna kisichowezekana kwako.
Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo lapenya mpaka mahali patakatifu mbinguni.
Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona, wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao.”
Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote. Enyi malaika wakuu, msifuni Mwenyezi-Mungu; mnaotimiza amri zake na kutekeleza neno lake! Enyi jeshi lote la mbinguni, msifuni Mwenyezi-Mungu; enyi watumishi wake mnaotekeleza matakwa yake! Msifuni Mwenyezi-Mungu enyi viumbe vyake vyote; msifuni popote mlipo katika milki yake. Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Ndiye anayenisamehe uovu wangu wote, na kuniponya magonjwa yote. Ndiye aniokoaye kutoka kifoni, na kunijalia rehema na fadhili zake.
Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’. Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza. Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’.
Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu.
Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini.
Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.
Kama tukiuzingatia ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa; chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga katika upendo.
Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.
Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo.
Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.”
Wewe umeniumba, mwili wangu wote; ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu. Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu; wewe wanijua kabisakabisa.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.
Wanionesha njia ya kufikia uhai; kuwako kwako kwanijaza furaha kamili, katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.
Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu.
“Nitawaongoza vipofu katika njia wasiyoifahamu, nitawaongoza katika njia ambazo hawazijui. Mbele yao giza nitaligeuza kuwa mwanga, na mahali pa kuparuza patakuwa laini. Huo ndio mpango wangu wa kufanya, nami nitautekeleza.
Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa.
Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu,
Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu.
“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu.
Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!” Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu.
Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uhai – uhai kamili.
Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote.
Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine kama wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote.
“Niite, nami nitakujibu na kukuambia mambo makubwa yaliyofichika ambayo hujapata kuyajua.
Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.
Umenifanya nione taabu nyingi ngumu, lakini utanirudishia tena uhai, wewe utaniinua tena kutoka huko chini. Utaniongezea heshima yangu, na kunifariji tena.
“Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba. “Basi, unapomsaidia maskini, usijitangaze. Usifanye kama wanafiki wafanyavyo katika masunagogi na njiani ili watu wawasifu. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia; walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu.
Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai. Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!
Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’”
Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.
Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu.
Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.
Basi, sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye.
Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima, nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida. Nitawaimarisha mwilini, nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji, kama chemchemi ya maji ambayo maji yake hayakauki kamwe.
Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu. Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini; hata kama bahari ikichafuka na kutisha, na milima ikatetemeka kwa machafuko yake.
Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu.
Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatia tuzo kubwa. Mnahitaji kuwa na uvumilivu ili muweze kutimiza matakwa ya Mungu na kupokea kile alichoahidi.
Bwana mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote.
Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha.
Imbeni kwa furaha, enyi mbingu! Shangilia ewe dunia. Pazeni sauti mwimbe enyi milima, maana Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, naam, atawaonea huruma watu wake wanaoteseka.
Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni.
Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.