Rafiki yangu, najua ya kwamba maisha yanaweza kuwa magumu sana. Wakati mwingine tunapatwa na shida na matatizo ambayo yanatufanya tujisikie kuzidiwa na huzuni. Tunaweza hata kusahau ahadi za Mungu kwetu.
Lakini katika nyakati hizi za mashaka, kumbuka kwamba Mungu yuko pamoja nasi kila wakati. Yeye ndiye anayeshikilia kila kitu mikononi mwake. Usikate tamaa! Usiache kumwamini Mungu mwema. Amini upendo wake na utunzaji wake kwako.
Hata kama unapitia magumu, unaweza kujificha chini ya mbawa zake. Ametuahidi kwamba atakuwa pamoja nasi siku zote, hadi mwisho wa dunia. Kama Biblia inavyosema katika Mathayo 28:20, "na, tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari."
Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Mwenyezi-Mungu ni mwema, yeye ni ngome ya usalama wakati wa taabu. Yeye huwalinda wote wanaokimbilia usalama kwake.
Silaha zote zilizoundwa kukudhuru wewe hazitafaa chochote kile. Mtu akikushtaki mahakamani, utamshinda. Hilo ndilo fungu nililowapangia watumishi wangu. Hizo ndizo haki nilizowathibitishia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Muwe imara na hodari, wala msiwaogope au kutishwa nao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ndiye anayekwenda pamoja nanyi. Yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa.”
Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.”
Hakuna mtu atakayekushinda siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe.
Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Aliisikia sauti yangu hekaluni mwake; kilio changu kilimfikia masikioni mwake.
Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo?
Afadhali kuwa na kidogo na kumcha Mwenyezi-Mungu, kuliko kuwa na mali nyingi pamoja na taabu.
Maana yeye hapuuzi au kudharau unyonge wa mnyonge; wala hajifichi mbali naye, ila humsikia anapomwomba msaada.
Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.” ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!” Hakika Mungu atakuokoa katika mtego; atakukinga na maradhi mabaya. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake; mkono wake utakulinda na kukukinga.
Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda.
“Abarikiwe mtu anayemtegemea Mwenyezi-Mungu, mtu ambaye Mwenyezi-Mungu ndiye tegemeo lake. Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya maji, upenyezao mizizi yake karibu na chemchemi. Hauogopi wakati wa joto ufikapo, majani yake hubaki mabichi. Hauhangaiki katika mwaka wa ukame, na hautaacha kuzaa matunda.
Siku ya taabu atanificha bandani mwake; atanificha katika hema lake, na kunisalimisha juu ya mwamba.
Sasa rudini nyumbani mkafanye sherehe, mle vinono na kunywa divai nzuri, lakini kumbukeni kuwapelekea wale ambao hawana cha kutosha; kwani leo ni siku takatifu kwa Bwana wetu. Msihuzunike kwa sababu furaha anayowajalia Mwenyezi-Mungu itawapeni nguvu.”
Hata kama mitini isipochanua maua, wala mizabibu kuzaa zabibu; hata kama mizeituni isipozaa zeituni, na mashamba yasipotoa chakula; hata kama kondoo wakitoweka zizini, na mifugo kukosekana mazizini, mimi nitaendelea kumfurahia Mwenyezi-Mungu nitamshangilia Mungu anayeniokoa.
Nitashangilia na kufurahia fadhili zako, maana wewe waiona dhiki yangu, wajua na taabu ya nafsi yangu.
Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia, na kuwaokoa katika taabu zao zote. Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo; huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu, na kuwalinda wakati wa taabu. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni. Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa; huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa, maana wanakimbilia usalama kwake.
Nilimngojea Mwenyezi-Mungu kwa uvumilivu, akanielekea na kukisikia kilio changu. Sikuuficha moyoni mwangu ukombozi ulionijalia, nimetangaza daima kuwa wewe ni mwokozi mwaminifu; sikulificha kusanyiko kubwa la watu fadhili zako na uaminifu wako. Ee Mwenyezi-Mungu, usininyime huruma yako! Fadhili zako na uaminifu wako vinihifadhi daima. Maafa yasiyohesabika yanizunguka, maovu yangu yanikaba hata siwezi kuona; ni mengi kuliko nywele kichwani mwangu, nami nimevunjika moyo. Upende ee Mwenyezi-Mungu kuniokoa; ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia. Wanaonuia kuniangamiza, na waaibike na kufedheheka! Hao wanaotamani niumie, na warudi nyuma na kuaibika! Hao wanaonisimanga, na wapumbazike kwa kushindwa kwao! Lakini wote wale wanaokutafuta wafurahi na kushangilia kwa sababu yako. Wapendao wokovu wako, waseme daima: “Mwenyezi-Mungu ni Mkuu!” Mimi ni maskini na fukara, ee Bwana; lakini ee Bwana wewe wanikumbuka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; uje, ee Mungu wangu, usikawie! Aliniondoa katika shimo la hatari, alinitoa katika matope ya dimbwi, akanisimamisha salama juu ya mwamba, na kuziimarisha hatua zangu.
Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako, naye atakutegemeza; kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.
Unihurumie, ee Mungu, unihurumie, maana kwako nakimbilia usalama. Kivulini mwa mabawa yako nitakimbilia usalama, hata hapo dhoruba ya maangamizi itakapopita.
Ninakulilia kutoka miisho ya dunia, nikiwa nimevunjika moyo. Uniongoze juu kwenye mwamba mkubwa maana wewe ndiwe kimbilio langu, kinga yangu imara dhidi ya adui.
Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu, kwake watoka wokovu wangu. Msitegemee dhuluma, msijisifie mali ya wizi; kama mali zikiongezeka, msizitegemee. Mungu ametamka mara moja, nami nimesikia tena na tena: Kwamba enzi ni mali yake Mungu; naam, nazo fadhili ni zake Bwana; humlipa kila mtu kadiri ya matendo yake. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika.
Umenifanya nione taabu nyingi ngumu, lakini utanirudishia tena uhai, wewe utaniinua tena kutoka huko chini. Utaniongezea heshima yangu, na kunifariji tena.
Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele.
Ee Mwenyezi-Mungu, mwokozi wangu, ninalia mchana kutwa, na usiku nakulalamikia. Je, wewe huwatendea wafu maajabu yako? Je, mizimu hufufuka na kukusifu? Je, fadhili zako zinatajwa kaburini, au uaminifu wako kwenye makao ya maangamizi? Je, maajabu yako yanajulikana humo gizani, au wema wako katika nchi ya waliosahauliwa? Lakini mimi nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu; kila asubuhi nakuletea ombi langu. Mbona ee Mwenyezi-Mungu wanitupilia mbali? Kwa nini unanificha uso wako? Nimeteseka na kukaribia kifo tangu ujana wangu; nateseka kwa mapigo yako, niko hoi kabisa. Ghadhabu yako imeniwakia; mashambulio yako ya kutisha yananiangamiza. Yananizunguka kama mafuriko mchana kutwa; yananizingira yote kwa pamoja. Umewafanya rafiki na wenzangu wote waniepe; giza ndilo limekuwa mwenzangu. Sala yangu ikufikie, usikilize kilio changu. Maafa mengi yamenipata, nami niko karibu kufa.
Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.” ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!”
Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu, na kilio changu kikufikie. kwa sababu ya ghadhabu na hasira yako, maana umeniokota na kunitupilia mbali. Maisha yangu ni kama kivuli cha jioni; ninanyauka kama nyasi. Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, watawala milele; jina lako lakumbukwa vizazi vyote. Wewe utainuka na kuurehemu mji wa Siyoni; maana wakati umefika wa kuutendea mema; wakati wake uliopangwa umefika. Watumishi wako wanauthamini sana, ujapokuwa magofu sasa; wanauonea huruma, ingawa umeharibika kabisa. Mataifa yataliheshimu jina la Mwenyezi-Mungu; wafalme wote duniani wataogopa utukufu wake. Mwenyezi-Mungu ataijenga upya Siyoni, na kuonekana alivyo mtukufu. Ataikubali sala ya fukara; wala hatayakataa maombi yao. Andika jambo hili kwa ajili ya vizazi vijavyo; watakaozaliwa baadaye wamsifu Mwenyezi-Mungu. Kwamba aliangalia chini kutoka patakatifu pake juu, Mwenyezi-Mungu aliangalia dunia kutoka mbinguni, Usijifiche mbali nami wakati wa taabu! Unitegee sikio lako, unijibu upesi wakati ninapokuomba!
Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu, naye akanisikia na kuniweka huru. Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu; binadamu ataweza kunifanya nini?
Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda; waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali; kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.
Ninapokaribia kukata tamaa kabisa, yeye yupo, anajua mwenendo wangu. Maadui wamenitegea mitego njiani mwangu.
Ee Mwenyezi-Mungu, unijibu haraka; maana nimekata tamaa kabisa! Usijifiche mbali nami, nisije nikawa kama wale washukao kwa wafu. Asubuhi unioneshe fadhili zako, maana nimekuwekea tumaini langu. Unifundishe mwenendo wa kufuata, maana nakuelekezea ombi la moyo wangu.
Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Maana wewe umekuwa ngome kwa maskini, ngome kwa fukara katika taabu zao. Wewe ni kimbilio wakati wa tufani, kivuli wakati wa joto kali. Kweli pigo la watu wakatili ni kali kama tufani inayopiga ukuta;
Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea.
Waambieni waliokufa moyo: “Jipeni moyo, msiogope! Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi, atakuja kuwaadhibu maadui zenu; atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.”
Yeye huwapa uwezo walio hafifu, wanyonge huwapa nguvu. Sauti ya mtu anaita jangwani: “Mtayarishieni Mwenyezi-Mungu njia, nyosheni barabara kuu kwa ajili ya Mungu wetu. Hata vijana watafifia na kulegea; naam, wataanguka kwa uchovu. Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’”
Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza.
Imbeni kwa furaha, enyi mbingu! Shangilia ewe dunia. Pazeni sauti mwimbe enyi milima, maana Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, naam, atawaonea huruma watu wake wanaoteseka.
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi, naam mimi, ndimi ninayekufariji. Kwa nini wewe unamwogopa mtu ambaye hufa, binadamu ambaye hutoweka kama nyasi?
Milima yaweza kutoweka, vilima vyaweza kuondolewa, lakini fadhili zangu hazitakuondoka, agano langu la amani halitaondolewa. Mimi Mwenyezi-Mungu nikuhurumiaye nimesema.
Wewe usiwaogope watu hao, kwa maana niko pamoja nawe kukulinda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye.
Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho. Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno.
Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele. Ingawa atufanya tuhuzunike, atakuwa na huruma tena kadiri ya wingi wa fadhili zake. Yeye hapendelei kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu.
Kondoo waliopotea nitawatafuta na waliotangatanga nitawarudisha nyumbani. Waliojeruhiwa nitawatibu, na wale walio dhaifu nitawapa nguvu. Kondoo wanono na wenye nguvu nitawaangamiza. Mimi nitawachunga kondoo kama itakiwavyo.
Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Hapo akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”
Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine?
“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu.
Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu.
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha; tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa.
Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.
Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu.
Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu.
Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
Huyu Kuhani Mkuu wetu anaelewa kabisa unyonge wetu; yeye mwenyewe alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.
Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?”
Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu. Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu. kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka, majaribio ambayo shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu, ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.
Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi.
Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
Palipo na upendo hapana woga; naam, upendo kamili hufukuza woga wote. Basi, mtu mwenye woga hajakamilika bado katika upendo, kwani woga huhusikana na adhabu.
Kwa kuwa wewe umezingatia neno langu la kuwa na uvumilivu thabiti, mimi nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima, kuwajaribu wote wanaoishi duniani.
Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena, kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uhai. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”
Yeye atayafuta machozi yao yote; maana kifo hakitakuwako tena, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!”
Kama mama amtulizavyo mwanawe, kadhalika nami nitawatuliza; mtatulizwa mjini Yerusalemu.
Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
Niliiona mienendo yao, lakini nitawaponya; nitawaongoza na kuwapa faraja, nitawatuliza hao wanaoomboleza. Mimi nitawapa amani, amani kwa walio mbali na walio karibu! Mimi nitawaponya.
“Katika taabu yangu, nilimwita Mwenyezi-Mungu; nilimwita Mungu wangu. Toka hekaluni mwake aliisikia sauti yangu, kilio changu kilimfikia masikioni mwake.