Zekaria 12 - Swahili Revised Union VersionUshindi wa Yerusalemu Uaguzi 1 Ufunuo wa neno la BWANA juu ya Israeli. Haya ndiyo asemayo BWANA, azitandaye mbingu, auwekaye msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake. 2 Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumbayumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu. 3 Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata majeraha mengi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake. 4 Katika siku hiyo, asema BWANA, nitamtia kila farasi ushangao, na yeye ampandaye nitamtia wazimu; nami nitaifunulia nyumba ya Yuda macho yangu, nami nitamtia upofu kila farasi wa hayo makabila ya watu. 5 Na wakuu wa Yuda watasema mioyoni mwao, Wenyeji wa Yerusalemu wana nguvu katika BWANA wa majeshi, Mungu wao. 6 Siku hiyo nitawafanya wakuu wa Yuda kuwa kama kigae chenye moto katika kuni, na kama kinga cha moto katika miganda; nao watateketeza watu wa kila kabila, wawazungukao pande zote, upande wa mkono wa kulia na upande wa mkono wa kushoto; na baada ya haya Yerusalemu utakaa mahali pake, naam, hapo Yerusalemu. 7 Naye BWANA ataziokoa hema za Yuda kwanza, ili utukufu wa nyumba ya Daudi, na utukufu wa wenyeji wa Yerusalemu, usipate kutukuzwa kuliko Yuda. 8 Katika siku hiyo BWANA atawalinda wenyeji wa Yerusalemu; na yeye aliye dhaifu miongoni mwao atakuwa kama Daudi siku hiyo; nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama malaika wa BWANA mbele yao. 9 Hata itakuwa siku hiyo, ya kwamba nitayaangamiza mataifa yote yatakayokuja kupigana na Yerusalemu. Kumuomboleza yule aliyedungwa 10 Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimdunga; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza. 11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido. 12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao; 13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao. 14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya