Zekaria 10 - Swahili Revised Union VersionMatengenezo ya Yuda na Israeli 1 Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA aletaye mawingu ya mvua, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi shambani. 2 Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo watu wanatangatanga kama kondoo, wanateseka kwa kukosa mchungaji. 3 Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani. 4 Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila kamanda. 5 Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu BWANA yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa. 6 Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni BWANA, Mungu wao, nami nitawasikia. 7 Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia BWANA. 8 Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyokua hapo awali. 9 Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi. 10 Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; hata pasiwe na nafasi ya kuwatosha. 11 Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka. 12 Nami nitawatia nguvu katika BWANA; nao watatembea huku na huko katika jina lake, asema BWANA. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya