Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yoshua 17 - Swahili Revised Union Version


Nusu nyingine ya kabila la Manase (magharibi)

1 Hii ndiyo sehemu waliyopewa kabila la Manase; maana, yeye alikuwa ni mzaliwa wa kwanza, wa Yusufu. Na Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase, babaye Gileadi, kwa sababu alikuwa mtu wa vita, basi alikuwa na Gileadi na Bashani.

2 Na kura ilikuwa ni ya hao wana wa Manase waliosalia kwa kufuata jamaa zao; kwa wana wa Abiezeri, kwa wana wa Heleki, kwa wana wa Asrieli, kwa wana wa Shekemu, kwa wana wa Heferi na kwa wana wa Shemida; hao ndio wana wa kiume wa Manase, mwana wa Yusufu, kwa kufuata jamaa zao.

3 Lakini Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana wa kiume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, Nuhu, Hogla, Milka na Tirza.

4 Nao wakaja mbele ya kuhani Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya viongozi, wakasema, BWANA alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuifuata hiyo amri ya BWANA akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao.

5 Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng'ambo ya Yordani;

6 kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe wa kiume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana wa kiume wa Manase waliosalia.

7 Mpaka wa Manase ulikuwa kutoka Asheri hadi Mikmeta, ulioelekea Shekemu; tena mpaka ukaendelea upande wa kulia, hata kuwafikia wenyeji wa Entapua.

8 Hiyo nchi ya Tapua ilikuwa ni mali ya Manase; lakini ule mji wa Tapua uliokuwa katika mpaka wa Manase ulikuwa ni mali ya wana wa Efraimu.

9 Tena mpaka uliteremka hadi kijito cha Kana, upande wa kusini wa hicho kijito; miji hiyo ilikuwa ya Efraimu kati ya miji ya Manase; na mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa hicho kijito, na mwisho wake ulikuwa baharini;

10 upande wa kusini ilikuwa ni mali ya Efraimu, na upande wa kaskazini ilikuwa ni mali ya Manase, na bahari ilikuwa mpaka wake; nao wakafika hadi Asheri upande wa kaskazini, na kufika hata Isakari upande wa mashariki.

11 Tena Manase alikuwa na miji katika Isakari na katika Asheri, nayo ni hii, Beth-sheani na vijiji vyake, Ibleamu na miji yake, wenyeji wa Dori na miji yake, wenyeji wa Endori na miji yake, wenyeji wa Taanaki na miji yake, wenyeji wa Megido na miji yake, na pia theluthi ya Nafathi.

12 Lakini wana wa Manase hawakuweza kuwafukuza wenyeji wa miji hiyo; bali hao Wakanaani walijikaza ili wakae katika nchi hiyo.

13 Kisha ikawa, hapo hao wana wa Israeli walipokuwa wamepata nguvu zaidi, ndipo wakawalazimisha hao Wakanaani wafanye kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa.


Kabila la Yusufu lateta

14 Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa mimi sehemu moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa kubwa la watu, kwa sababu BWANA amenibariki hata hivi sasa?

15 Yoshua akawaambia, Kwa kuwa wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; maana hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi.

16 Wana wa Yusufu wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Beth-sheani na miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia.

17 Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata sehemu moja tu;

18 lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa sasa ni msitu, wewe utaufyeka, na kuimiliki yote hadi mwisho wake; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, wajapokuwa wana magari ya chuma, wajapokuwa ni wenye uwezo.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo