Mwanzo 16 - Swahili Revised Union VersionKuzaliwa kwa Ishmaeli 1 Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. 2 Sarai akamwambia Abramu, kwa kuwa BWANA amenifunga tumbo nisizae, sasa mwingilie mjakazi wangu, labda nitapata uzao kutoka kwake. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. 3 Kwa hiyo, baada ya Abramu kukaa miaka kumi katika nchi ya Kanaani, Sarai mkewe Abramu alimtwaa Hajiri Mmisri, mjakazi wake, akampa Abramu mumewe, kama mke. 4 Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bimkubwa alikuwa duni machoni pake. 5 Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. 6 Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mikononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. 7 Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. 8 Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, na unakwenda wapi? Akanena, Namkimbia bimkubwa wangu Sarai. 9 Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bimkubwa wako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. 10 Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. 11 Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. 12 Naye atakuwa kama punda mwitu kati ya watu, mkono wake utapingana na watu wote na mkono wa kila mtu ukipingana naye; na ataishi kwa ugomvi na jamaa yake yote. 13 Akampa jina BWANA aliyesema naye, “Wewe U Mungu uonaye,” kwani alisema, “Kweli nimemwona Mungu na nikaendelea kuishi baada ya kumuona?” 14 Kwa hiyo kisima kile kiliitwa Beer-lahai-roi. Tazama, kiko kati ya Kadeshi na Beredi. 15 Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume; Abramu akamwita jina lake Ishmaeli, yule mwanawe, ambaye Hajiri alimzaa. 16 Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajiri alipomzalia Abramu Ishmaeli. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya