Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mathayo 28 - Swahili Revised Union Version


Kufufuka kwa Yesu

1 Na sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.

2 Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la ardhi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia.

3 Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji.

4 Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.

5 Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.

6 Hayupo hapa; maana amefufuka kama alivyosema. Njooni, mpatazame mahali alipolazwa.

7 Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.

8 Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari.

9 Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia.

10 Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; nendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.


Ripoti ya walinzi

11 Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya walinzi waliingia mjini, wakawaambia wakuu wa makuhani juu ya mambo yote yaliyotendeka.

12 Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi,

13 wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala.

14 Na jambo hili likisikika kwa mtawala, sisi tutasema naye, nanyi hamtapata shida.

15 Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.


Kutumwa kwa wanafunzi

16 Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya hadi katika mlima ule aliowaagiza Yesu.

17 Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao walikuwa na mashaka.

18 Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

19 Basi, nendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo