Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hesabu 36 - Swahili Revised Union Version


Wanawake walioolewa na urithi wao

1 Kisha wale wakuu wa nyumba za mababa ya jamaa ya wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, katika jamaa za wana wa Yusufu, wakakaribia, na kunena mbele ya Musa, na mbele ya wakuu walio juu ya nyumba za mababa ya wana wa Israeli;

2 wakasema, BWANA alimwagiza bwana wangu awape wana wa Israeli nchi kwa kupiga kura iwe urithi wao; tena bwana wangu aliagizwa na BWANA awape binti za Selofehadi ndugu yetu huo urithi wa baba yao.

3 Wakiolewa na watu wa wana wa hayo makabila mengine ya wana wa Israeli, ndipo urithi wao utatwaliwa na kuondolewa katika urithi wa baba zetu, na hilo kabila watakalotiwa ndani yake litaongezewa urithi wao; basi urithi huo utaondolewa katika kura ya urithi wetu.

4 Tena itakapokuwapo hiyo jubilii ya wana wa Israeli, ndipo urithi wa hilo kabila ambalo wamekuwa ndani yake utaongezewa huo urithi wao; hivyo urithi wao utaondolewa katika urithi wa kabila la baba zetu.

5 Basi Musa akawaagiza wana wa Israeli kama neno la BWANA lilivyokuwa, akasema, Kabila la wana wa Yusufu imenena yaliyo haki.

6 BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila la baba zao.

7 Hivyo hapana urithi wowote wa wana wa Israeli utakaotoka kabila hili kwenda kabila hili; kwa kuwa wana wa Israeli watashikamana kila mtu na urithi wa kabila la baba zake.

8 Na kila binti atakayemiliki urithi katika kabila lolote katika wana wa Israeli, ataolewa katika jamaa moja ya kabila la baba yake, ili wana wa Israeli wapate kumiliki kila mtu urithi wa baba zake.

9 Hivyo hapatakuwa na urithi wowote utakaotoka kabila hili kwenda kabila hili; kwa kuwa makabila ya wana wa Israeli yatashikamana kila mmoja na urithi wake mwenyewe.

10 Basi hao binti za Selofehadi wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Musa;

11 kwa kuwa Mala, na Tirza, na Hogla, na Milka, na Nuhu, binti za Selofehadi waliolewa na wanaume, wana wa ndugu za baba yao.

12 Waliolewa katika jamaa za wana wa Manase, mwana wa Yusufu, na urithi wao ukakaa katika kabila la jamaa ya baba yao.

13 Haya ndiyo maagizo na hukumu, ambayo BWANA aliwaagiza wana wa Israeli, kwa mkono wa Musa, hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo