1 Samueli 6 - Swahili Revised Union VersionSanduku la Agano larudishwa Israeli 1 Basi, hilo sanduku la BWANA lilikuwamo katika nchi ya Wafilisti muda wa miezi saba. 2 Nao Wafilisti wakawaita makuhani na waaguzi, wakasema, Tulifanyieje sanduku la BWANA? Tuonesheni jinsi tuwezavyo kulirudisha mahali pake. 3 Nao wakajibu, Mkilirudisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe kitupu; lakini msikose kumpelekea na matoleo ya kosa; hivyo mtapona, tena mtafunuliwa ni kwa sababu gani mkono wake haukuondolewa kwenu. 4 Ndipo wakauliza, Na hayo matoleo ya kosa tutakayompelekea, yatakuwa ya namna gani? Na yawe majipu ya dhahabu matano, na panya wa dhahabu watano, sawasawa na idadi ya wakuu wa Wafilisti; kwa kuwa tauni moja ilikuwa juu yenu nyote, na juu ya wakuu wenu. 5 Kwa hiyo mtafanya sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu wanaoiharibu nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu. 6 Mbona, basi, mnaifanya mioyo yenu migumu, kama vile wale Wamisri, na yule Farao, walivyoifanya mioyo yao migumu? Hata na hao, baada ya kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu waende, nao wakaondoka? 7 Basi sasa jifanyieni gari jipya, mtwae na ng'ombe wake wawili wakamwao, ambao hawajafungwa nira, nanyi mkawafunge hao ng'ombe garini, na kuwaondoa ndama wao na kuwatia zizini; 8 kisha, litwaeni hilo sanduku la BWANA, na kuliweka juu ya gari; na hivyo vitu vya dhahabu, mtakavyompelekea kuwa matoleo ya kosa, mvitie katika kasha kando yake; mkalipeleke sanduku, lipate kwenda. 9 Kisha angalieni, likikwea kwa njia ya mpakani mwake kwenda Beth-shemeshi, basi, ndiye aliyetutenda uovu huo mkuu; la, sivyo, ndipo tutakapojua ya kwamba si mkono wake uliotupiga; ilikuwa ni bahati mbaya iliyotupata. 10 Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng'ombe wawili wakamuliwao, wakawafunga garini, na ndama wao wakawafunga zizini; 11 kisha wakaliweka sanduku la BWANA juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao. 12 Na hao ng'ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kulia wala wa kushoto; na wakuu wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi. 13 Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona. 14 Na lile gari likaingia katika konde la Yoshua wa Beth-shemeshi, na kusimama pale pale, palipokuwapo jiwe kubwa; basi wakaipasua miti ya lile gari, wakawatoa wale ng'ombe kuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. 15 Nao Walawi walilishusha sanduku la BWANA, na lile kasha lililokuwa pamoja nalo, lenye vile vitu vya dhahabu; wakaviweka juu ya lile jiwe kubwa; nao watu wa Beth-shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja dhabihu siku iyo hiyo kwa BWANA. 16 Na hao wakuu watano wa Wafilisti, hapo walipoyaona hayo, walirejea Ekroni siku iyo hiyo. 17 Hii ndiyo hesabu ya yale majipu waliyoyapeleka wale Wafilisti, yawe matoleo ya kosa kwa BWANA; kwa Ashdodi moja, kwa Gaza moja, kwa Ashkeloni moja, kwa Gathi moja, na kwa Ekroni moja; 18 na panya wa dhahabu, kwa idadi ya miji yote ya Wafilisti, milki zao wale wakuu watano, miji yenye maboma na vijiji vya mashamba pia. Nalo lile jiwe kubwa, ambalo juu yake waliliweka sanduku la BWANA, liko hata hivi leo hapo kondeni pa Yoshua wa Beth-shemeshi. Sanduku la Mungu katika Kiriath-yearimu 19 Basi BWANA aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la BWANA, wapata watu sabini, na watu elfu hamsini; nao watu wakalalamika, kwa kuwa BWANA amewapiga watu kwa uuaji mkuu. 20 Nao watu wa Beth-shemeshi wakasema, Ni nani awezaye kusimama mbele za BWANA, huyu Mungu mtakatifu? Naye atapanda kwenda kwa nani kutoka kwetu? 21 Nao wakatuma wajumbe waende kwa wenyeji wa Kiriath-yearimu, kusema, Wafilisti wamelirudisha sanduku la BWANA; basi shukeni, mkalichukue. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya