Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia, na kuwaokoa katika taabu zao zote. Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo; huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda.
Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako, naye atakutegemeza; kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza.
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Nampenda Mwenyezi-Mungu, kwa maana anisikia, maana amesikia kilio cha ombi langu. Nilikuwa na imani hata niliposema: “Mimi nimetaabika mno.” Hata nilisema kwa hofu yangu: “Binadamu wote hawaaminiki!” Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu wote alionitendea? Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa, nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu. Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu, mbele ya watu wake wote. Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu si jambo dogo mbele yake. Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako; ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako; umenifungulia vifungo vyangu. Nitakutolea tambiko za shukrani, na kukupa heshima zangu. Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu mbele ya watu wako wote, waliokusanyika hekaluni mwako, katikati ya Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Yeye amenitegea sikio, hivyo nitamwomba muda wote niishio.
Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.
Yeye atayafuta machozi yao yote; maana kifo hakitakuwako tena, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!”
Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea.
Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mkombozi wangu; Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu.
Bwana mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote.
Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Bwana Mwenyezi-Mungu amenijaza roho yake, maana Mwenyezi-Mungu ameniweka wakfu, akanituma niwaletee wanaokandamizwa habari njema, niwatibu waliovunjika moyo, niwatangazie mateka kwamba watapata uhuru, na wafungwa kwamba watafunguliwa. Nitafurahi sana kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, nafsi yangu itashangilia kwa sababu ya Mungu wangu. Maana amenivika vazi la wokovu, amenivalisha vazi la uadilifu, kama bwana arusi ajipambavyo kwa shada la maua, kama bibi arusi ajipambavyo kwa johari zake. Hivyo, kama vile ardhi ioteshavyo mimea, na shamba lichipushavyo mbegu zilizopandwa humo, Mwenyezi-Mungu atasababisha uadilifu na sifa kuchomoza mbele ya mataifa yote. Amenituma niutangaze mwaka wake wa neema, na siku ya Mungu wetu ya kulipiza kisasi; niwafariji wote wanaoomboleza; niwape wale wanaoomboleza katika Siyoni taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya moyo mzito. Nao wataitwa mialoni madhubuti, aliyopanda Mwenyezi-Mungu kuonesha utukufu wake.
“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai. Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!
Umenifanya nione taabu nyingi ngumu, lakini utanirudishia tena uhai, wewe utaniinua tena kutoka huko chini. Utaniongezea heshima yangu, na kunifariji tena.
Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu, humlinda yule ampendezaye. Ajapoanguka, haanguki akabaki chini, kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza.
Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.”
Palipo na upendo hapana woga; naam, upendo kamili hufukuza woga wote. Basi, mtu mwenye woga hajakamilika bado katika upendo, kwani woga huhusikana na adhabu.
Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?”
Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu, ningalikwisha angamia kwa taabu zangu. Sitasahau kamwe kanuni zako, maana kwa hizo umenipa uhai.
Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu.
Imbeni kwa furaha, enyi mbingu! Shangilia ewe dunia. Pazeni sauti mwimbe enyi milima, maana Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake, naam, atawaonea huruma watu wake wanaoteseka.
Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.
Mwenyezi-Mungu ndiye anayewaongoza; yeye atakuwa pamoja nanyi; yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa. Hivyo, msiogope wala msifadhaike.”
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima.
“Mtatoka Babuloni kwa furaha; mtaongozwa mwende kwa amani. Milima na vilima mbele yenu vitapaza sauti na kuimba, na miti yote mashambani itawapigia makofi.
Wanaopanda kwa machozi, watavuna kwa shangwe. Wanaokwenda kupanda mbegu wakilia, watarudi kwa furaha wakichukua mavuno.
Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho. Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno.
Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele.
Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili.
Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu,
Lakini akaniambia: “Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu.” Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu.
Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye.
Mbona ninahuzunika hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu? Nitamtumainia Mungu, nitamsifu tena yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.
Maana ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu.
Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka, majaribio ambayo shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu, ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.
Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu, naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo
Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba, wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu. Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha; husikia kilio chao na kuwaokoa.
“Ndiyo maana nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa mwituni: Hawapandi, hawavuni, wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, nyinyi si wa thamani kuliko hao?
Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika.
Waliokombolewa na Mwenyezi-Mungu watarudi, watakuja Siyoni wakipiga vigelegele. Watakuwa wenye furaha ya milele, watajaliwa furaha na shangwe; huzuni na kilio vitatoweka kabisa.
Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika. Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga. Niamkapo, bado nipo pamoja nawe.
Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.
Nyinyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.
Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu. Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu. kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru.
Hivi ndivyo asemavyo Mungu aliye juu kabisa, aishiye milele na ambaye jina lake ni “Mtakatifu”: “Mimi nakaa huko juu, mahali patakatifu, nakaa pia na wenye majuto na wanyenyekevu. Mimi nitawatia moyo walio wanyenyekevu na kuwapa nguvu wenye majuto.
Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
Mwenyezi-Mungu huwaangalia wale wamchao, watu ambao wanatumainia fadhili zake. Yeye huwaokoa katika kifo, huwaweka hai wakati wa njaa.
maana wewe umenisaidia daima. Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia. Roho yangu inaambatana nawe kabisa, mkono wako wa kulia wanitegemeza.
Ndipo wasichana wao watafurahi na kucheza, vijana na wazee watashangilia kwa furaha. Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha, nitawafariji na kuwapa furaha badala ya huzuni.
Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote.
Kama ningeliomba giza linifunike, giza linizunguke badala ya mwanga, kwako giza si giza hata kidogo, na usiku wangaa kama mchana; kwako giza na mwanga ni mamoja.
Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema: “Mkinirudia na kutulia mtaokolewa; kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.” Lakini nyinyi hamkutaka.
Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka.
Nitafurahi sana kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, nafsi yangu itashangilia kwa sababu ya Mungu wangu. Maana amenivika vazi la wokovu, amenivalisha vazi la uadilifu, kama bwana arusi ajipambavyo kwa shada la maua, kama bibi arusi ajipambavyo kwa johari zake.
Siku ya taabu atanificha bandani mwake; atanificha katika hema lake, na kunisalimisha juu ya mwamba.
Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha; tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda.
Kama mama amtulizavyo mwanawe, kadhalika nami nitawatuliza; mtatulizwa mjini Yerusalemu.
Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye.
Heri watu wanaojua kukushangilia, wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu. Wanafurahi mchana kutwa kwa sababu yako, na kukusifu kwa ajili ya uadilifu wako.
Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri nyinyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha.
Nitapaza sauti kwa furaha, ninapokuimbia wewe sifa zako, na roho yangu itakusifu maana umeniokoa.
Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
Ee Mwenyezi-Mungu, utuonee huruma, kwako tumeliweka tumaini letu. Uwe kinga yetu kila siku, wokovu wetu wakati wa taabu.
Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe. Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa.
Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatia tuzo kubwa. Mnahitaji kuwa na uvumilivu ili muweze kutimiza matakwa ya Mungu na kupokea kile alichoahidi.
Mwenyezi-Mungu atanijalia fadhili zake mchana; nami nimwimbie wimbo wa sifa usiku, nimwombe Mungu anipaye uhai.
Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu.
Hapo tuliangua kicheko; tulishangilia kwa furaha. Nao watu wa mataifa mengine walisema: “Mwenyezi-Mungu amewatendea mambo makubwa!” Kweli Mwenyezi-Mungu alitutendea mambo makubwa, tulifurahi kwelikweli!
Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu.
Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia; walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Je, mama aweza kumsahau mwanawe anayenyonya, asimwonee huruma mtoto wa tumbo lake? Hata kama mama aweza kumsahau mwanawe, mimi kamwe sitakusahau. Nimekuchora katika viganja vyangu; kuta zako naziona daima mbele yangu.
Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uhai.”
Fadhili zako ni bora kuliko maisha, nami nitakusifu kwa mdomo wangu. Nitakushukuru maisha yangu yote; nitainua mikono yangu na kukuomba.
Mwenyezi-Mungu, Mungu wako yu pamoja nawe yeye ni shujaa anayekuletea ushindi. Yeye atakufurahia kwa furaha kuu, kwa upendo wake atakujalia uhai mpya. Atakufurahia kwa wimbo wa sauti kubwa,
Ee Mwenyezi-Mungu, matendo yako yanifurahisha; nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda.
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote.
Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana, mwombeni msaada wakati yupo bado karibu. Waovu na waache njia zao mbaya, watu wabaya waachane na mawazo yao mabaya; wamrudie Mwenyezi-Mungu apate kuwahurumia, wamwendee Mungu wetu maana atawasamehe.
Ninakulilia kutoka miisho ya dunia, nikiwa nimevunjika moyo. Uniongoze juu kwenye mwamba mkubwa maana wewe ndiwe kimbilio langu, kinga yangu imara dhidi ya adui.
Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini.
Kama paa atamanivyo maji ya kijito, ndivyo ninavyokutamani, ee Mungu wangu! Nimepondwa kwa matukano yao, wanaponiuliza kila siku: “Yuko wapi, Mungu wako!” Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu. Naona kiu ya Mungu, kiu ya Mungu aliye hai. Nitafika lini kwake na kuuona uso wake?
kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe.
Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.
Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu; yeye hutuneemesha na kutujalia fahari. Hawanyimi chochote kilicho chema, wale waishio kwa unyofu.
Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.”
Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake, atawabeba kifuani pake, na kondoo wanyonyeshao atawaongoza polepole.
Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu.
Jinsi gani ulivyo mwingi wema wako, uliowawekea wale wanaokucha! Wanaokimbilia usalama kwako wawapa mema binadamu wote wakiona.
Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza.
Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote.
Wewe wakujua kusukwasukwa kwangu; waweka kumbukumbu ya machozi yangu yote. Je, yote si yamo kitabuni mwako?
Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao. Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni.
Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote?
Mwenyezi-Mungu ni mwema; fadhili zake zadumu milele, na uaminifu wake katika vizazi vyote.
Naomba nikae nyumbani mwako milele nipate usalama chini ya mabawa yako. Ee Mungu, umezisikia ahadi zangu, umenijalia sehemu yangu unayowapa wale wakuchao.