Rafiki yangu, unapojifunga siku, ni vizuri kuchukua muda kidogo kumshukuru Mungu kwa siku inayokwisha na kumwomba ulinzi wake kwa usiku unaokuja.
Najua usiku unaweza kuwa mzito kwetu. Shida za maisha, mambo ambayo hayajaenda vizuri, hali zinazotuzonga mchana kutwa, au hata magonjwa yanayotutia giza usiku. Lakini kumbuka, kama vile mitume walivyokuwa na Yesu pale kwenye ile boti, naye akalala usingizi, sisi pia hatuko peke yetu.
Kabla ya kulala, jaribu kusoma Biblia kidogo. Ina nguvu ya kutuliza mioyo yetu na kutupa amani. Ukweli wa neno la Mungu utabaki nawe usiku kucha, ukikupa amani ya Kristo. Inaweza kubadilisha hali yoyote ile.
Kama vile Yesu alivyokuwa na wanafunzi wake kwenye ile boti na akatuliza dhoruba, vivyo hivyo yuko nawe. Usihofu. Amani iwe nawe.
Unilinde ee Mungu; maana kwako nakimbilia usalama. Naam wewe hutaiacha nafsi yangu kuzimu, hutaniacha mimi mwaminifu wako nipate kuoza. Wanionesha njia ya kufikia uhai; kuwako kwako kwanijaza furaha kamili, katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele. Namwambia Mungu: “Wewe u Bwana wangu; sina jema lolote ila wewe.”
Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea.
Hatakuacha uanguke; mlinzi wako hasinzii. Kweli mlinzi wa Israeli hasinzii wala halali.
Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.” ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!”
sitakubali kulala usingizi, wala kusinzia; mpaka nikupatie wewe Mwenyezi-Mungu mahali pa kukaa, makao yako, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo!”
Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
Bwana mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote.
Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe ameshiba au amekula kidogo tu. Lakini usingizi wa tajiri ni wa wasiwasi daima, maana ziada ya mali yake humsumbua usiku kucha.
Mara maneno yako yalipofika, niliyameza; nayo yakanifanya niwe na furaha, yakawa utamu moyoni mwangu, maana mimi najulikana kwa jina lako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.
Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi na kuchelewa kwenda kupumzika jioni, mjipatie chakula kwa jasho lenu. Mungu huwaruzuku walio wake hata walalapo.
Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunipumzisha kwenye malisho mabichi; huniongoza kando ya maji matulivu, na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya. Huniongoza katika njia sawa kwa hisani yake.
Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu, kwake watoka wokovu wangu. Msitegemee dhuluma, msijisifie mali ya wizi; kama mali zikiongezeka, msizitegemee. Mungu ametamka mara moja, nami nimesikia tena na tena: Kwamba enzi ni mali yake Mungu; naam, nazo fadhili ni zake Bwana; humlipa kila mtu kadiri ya matendo yake. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika.
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda; waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali; kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza, usiku dhamiri yangu yanionya. Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima; yuko pamoja nami, wala sitatikisika.
Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi; usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa, watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya.
Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima.
Hana haja ya kuogopa akipata habari mbaya; ana moyo thabiti na humtegemea Mwenyezi-Mungu.
Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako, naye atakutegemeza; kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.
Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.
Hebu nisikie anachosema Mwenyezi-Mungu; maana anaahidi kuwapa watu wake amani, watu wake mwenyewe wasiporudia upuuzi wao
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima.
Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso zao. Aliifanya ile dhoruba kali itulie, nayo mawimbi yakanyamaza. akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni: Kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu; akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea.
Palipo na upendo hapana woga; naam, upendo kamili hufukuza woga wote. Basi, mtu mwenye woga hajakamilika bado katika upendo, kwani woga huhusikana na adhabu.
Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema, upate kuishi katika nchi na kuwa salama. Mtu mwadilifu husema maneno ya hekima, kwa ulimi wake hunena yaliyo ya haki. Huizingatia moyoni mwake sheria ya Mungu wake; naye hatetereki katika mwenendo wake. Mtu mwovu humvizia mtu mwema na kujaribu kumuua; lakini Mwenyezi-Mungu hatamtia mtu mwema makuchani mwake, wala kumwacha apatilizwe akishtakiwa. Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kushika njia yake, naye atakukuza uimiliki nchi, na kuwaona waovu wakiangamizwa. Nilimwona mwovu mdhalimu sana, alijiweka juu ya wote kama mierezi ya Lebanoni! Baadaye nikapita hapo, naye hakuwapo tena; nikamtafuta, lakini hakuonekana tena. Mwangalie mtu mwema, mtu mwadilifu; mtu anayependa amani hujaliwa wazawa. Lakini wakosefu wote wataangamizwa; na wazawa wao watafutiliwa mbali. Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu, na kuwalinda wakati wa taabu. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni.
“Ndiyo maana nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi?
Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku! Yeye hutubebea mizigo yetu; yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu.
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku, wala shambulio la ghafla mchana; huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku, wala maafa yanayotokea mchana.
Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.”
Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu, unipime, uyajue mawazo yangu. Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya, uniongoze katika njia ya milele.
Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema. Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, siku ile ya Bwana inakaribia.
Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni kuushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara.
Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha.
Ee Mungu, usikie kilio changu, usikilize sala yangu. Ninakulilia kutoka miisho ya dunia, nikiwa nimevunjika moyo. Uniongoze juu kwenye mwamba mkubwa
Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza.
Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu,
Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote.
Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.
Mungu mwenyewe anayetupatia amani awatakase nyinyi kabisa kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu – roho, mioyo na miili yenu – mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
Shomoro wawili huuzwa kwa sarafu moja ndogo. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu.
Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Wanaokujua wewe, ee Mungu hukutegemea, wewe Mwenyezi-Mungu huwatupi wakutafutao. Mwimbieni sifa Mwenyezi-Mungu akaaye Siyoni. Yatangazieni mataifa mambo aliyotenda! Mungu hulipiza kisasi kwa umwagaji damu; kamwe hasahau kilio cha wanaoonewa. Unirehemu, ee Mwenyezi-Mungu! Ona mateso ninayoteswa na wanaonichukia; wewe waninyakua kutoka nguvu za kifo, nisimulie sifa zako mbele ya watu wa Siyoni, nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa. Watu wa mataifa wametumbukia katika shimo walilochimba, wamenaswa miguu katika wavu waliouficha. Mwenyezi-Mungu amejionesha alivyo; ametekeleza hukumu. Watu waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe. Waovu wataishia kuzimu; naam, mataifa yote yanayomsahau Mungu. Lakini fukara hawatasahauliwa daima; tumaini la maskini halitapotea milele. Inuka, ee Mwenyezi-Mungu! Usimwache binadamu ashinde. Uyakusanye mataifa mbele yako, uyahukumu. Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako; nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu.
Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda.
Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru.
Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu. Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini;
Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Heri mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu, anayefurahia sana kutii amri zake. Watu waovu huona hayo na kuudhika; husaga meno kwa chuki na kutoweka, matazamio ya mtu mbaya huishia patupu. Wazawa wake watakuwa wenye nguvu nchini; watoto wa wanyofu watapata baraka. Nyumbani kwake kutakuwa na mali nyingi; uadilifu wake wadumu milele.
Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu; unifundishe nifuate unayotaka. Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha, kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu; ninakutegemea wewe kila siku.
niwape wale wanaoomboleza katika Siyoni taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya moyo mzito. Nao wataitwa mialoni madhubuti, aliyopanda Mwenyezi-Mungu kuonesha utukufu wake.
Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu,
Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito, unaozaa matunda kwa wakati wake, na majani yake hayanyauki. Kila afanyalo hufanikiwa.
Ee Mwenyezi-Mungu, utatimiza yote uliyoniahidi. Fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zadumu milele. Usisahau kazi ya mkono wako mwenyewe.
Milima yaweza kutoweka, vilima vyaweza kuondolewa, lakini fadhili zangu hazitakuondoka, agano langu la amani halitaondolewa. Mimi Mwenyezi-Mungu nikuhurumiaye nimesema.
Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu na mkombozi wangu!