Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako, naye atakutegemeza; kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
“Abarikiwe mtu anayemtegemea Mwenyezi-Mungu, mtu ambaye Mwenyezi-Mungu ndiye tegemeo lake. Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya maji, upenyezao mizizi yake karibu na chemchemi. Hauogopi wakati wa joto ufikapo, majani yake hubaki mabichi. Hauhangaiki katika mwaka wa ukame, na hautaacha kuzaa matunda.
Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
Bali, shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu na matakwa yake, na hayo yote mtapewa kwa ziada.
Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea. Mtumaini Mwenyezi-Mungu siku zote kwa maana yeye ni mwamba wa usalama milele.
Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu; kwake naliweka tumaini langu. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika. Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu; mwamba wangu mkuu na kimbilio langu ni Mungu. Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu.
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
“Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami nikiwa ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote.
Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunipumzisha kwenye malisho mabichi; huniongoza kando ya maji matulivu,
Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kumtumainia mwanadamu. Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kuwatumainia viongozi wa dunia.
Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.
Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru.
Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
Mimi ni maskini na fukara, ee Bwana; lakini ee Bwana wewe wanikumbuka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; uje, ee Mungu wangu, usikawie!
Anachofanya Mungu hakina dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia.
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima.
Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.” ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!”
Ee Mungu Mkuu, hofu inaponishika, mimi nakutumainia wewe. Namtumainia Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu dhaifu atanifanya nini?
Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza.
“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu.
Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’”
Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.
Hana haja ya kuogopa akipata habari mbaya; ana moyo thabiti na humtegemea Mwenyezi-Mungu. Yuko imara moyoni, wala hataogopa; naye atawaona maadui zake wanashindwa.
Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Muwe imara na hodari, wala msiwaogope au kutishwa nao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ndiye anayekwenda pamoja nanyi. Yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa.”
Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?”
Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu; unifundishe nifuate unayotaka. Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha, kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu; ninakutegemea wewe kila siku.
Mungu asema: “Nitakufunza na kukuonesha njia unayopaswa kufuata. Nitakushauri kwa uangalifu mkubwa.
Mioyo yetu yamtumainia Mwenyezi-Mungu. Yeye ni msaada wetu na ngao yetu. Naam twafurahi kwa sababu yake; tuna matumaini katika jina lake takatifu.
Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria;
Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.
Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu na mkombozi wangu; Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu.
Nani kati yenu amchaye Mwenyezi-Mungu? Nani anayetii maneno ya mtumishi wake? Kama yupo atembeaye gizani bila taa, amtumainie Mwenyezi-Mungu, na kumtegemea Mungu wake.
Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!”
Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
Unihurumie, ee Mungu, unihurumie, maana kwako nakimbilia usalama. Kivulini mwa mabawa yako nitakimbilia usalama, hata hapo dhoruba ya maangamizi itakapopita. Fadhili zako zaenea hata juu ya mbingu, uaminifu wako wafika hata mawinguni. Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote! Namlilia Mungu Mkuu, Mungu anikamilishiaye nia yake.
Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.
Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe.
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote.
Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.”
Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.
Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema: “Mkinirudia na kutulia mtaokolewa; kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.” Lakini nyinyi hamkutaka.
Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema.
Nalala na kupata usingizi, naamka tena maana wewe ee Mwenyezi-Mungu wanitegemeza. Sitayaogopa maelfu ya watu, wanaonizingira kila upande.
Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu, humlinda yule ampendezaye. Ajapoanguka, haanguki akabaki chini, kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza.
Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele.
Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mawazo yangu si kama mawazo yenu, wala njia zangu si kama njia zenu. Kama vile mbingu zilivyo mbali na dunia, ndivyo njia zangu zilivyo mbali na zenu, na mawazo yangu mbali na mawazo yenu.
Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu; yeye hutuneemesha na kutujalia fahari. Hawanyimi chochote kilicho chema, wale waishio kwa unyofu.
Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu. Nasema: “Wewe ni Mungu wangu!” Maisha yangu yamo mikononi mwako; uniokoe na maadui zangu, niokoe na hao wanaonidhulumu.
Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote.
Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
Usiogope juu ya tishio la ghafla, wala shambulio kutoka kwa waovu, Maana Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekutegemeza; atakuepusha usije ukanaswa mtegoni.
Bwana Mungu hunisaidia, kwa hiyo siwezi kufadhaika. Uso wangu nimeukaza kama jiwe; najua kwamba sitaaibishwa.
Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu, na kuniondoa katika hofu zangu zote. Mgeukieni Mungu mpate kufurahi; nanyi hamtaaibishwa kamwe.
Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.
Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza. Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba hutupatia yote tunayomwomba.
Nampenda Mwenyezi-Mungu, kwa maana anisikia, maana amesikia kilio cha ombi langu. Nilikuwa na imani hata niliposema: “Mimi nimetaabika mno.” Hata nilisema kwa hofu yangu: “Binadamu wote hawaaminiki!” Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu wote alionitendea? Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa, nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu. Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu, mbele ya watu wake wote. Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu si jambo dogo mbele yake. Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako; ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako; umenifungulia vifungo vyangu. Nitakutolea tambiko za shukrani, na kukupa heshima zangu. Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu mbele ya watu wako wote, waliokusanyika hekaluni mwako, katikati ya Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi-Mungu! Yeye amenitegea sikio, hivyo nitamwomba muda wote niishio.
Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana.
Ee Mwenyezi-Mungu, utuonee huruma, kwako tumeliweka tumaini letu. Uwe kinga yetu kila siku, wokovu wetu wakati wa taabu.
Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu.
Lakini mimi nazitumainia fadhili zako; moyo wangu na ufurahie wokovu wako. Nitakuimbia wewe, ee Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu mwingi ulionitendea!
Nilifanya hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya binadamu.
Lakini, kwangu ni vema kuwa karibu na Mungu, wewe Bwana Mwenyezi-Mungu ndiwe usalama wangu. Nitatangaza mambo yote uliyotenda!
Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye.
Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu.
Lakini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatukuzwa. Yeye huonesha ukuu wake kwa matendo yake ya haki, kwa kuwahukumu watu wake.
Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege!
Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa rehema na huruma; wewe ni mvumilivu, mwingi wa fadhili na uaminifu.
Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu.
Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu:
Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu, unipime, uyajue mawazo yangu. Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya, uniongoze katika njia ya milele.
Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia. Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu; naam, huwafundisha hao njia yake.
Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima, nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida. Nitawaimarisha mwilini, nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji, kama chemchemi ya maji ambayo maji yake hayakauki kamwe.
Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku! Yeye hutubebea mizigo yetu; yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu.
Kichwani mwa mtu mna mipango mingi, lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika.
Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.
Lakini mimi ni kama mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu. Nazitegemea fadhili zake milele na milele.
Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka, majaribio ambayo shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu, ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.
Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, dharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu.
Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
Katika kuungana na Kristo, sisi tumerithishwa wokovu kama tulivyopangiwa kadiri ya azimio lake Mungu atekelezaye kila kitu kulingana na uamuzi na matakwa yake.
Yahazieli akasema, “Sikilizeni watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu na mfalme Yehoshafati, Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: Msiogope wala msihangaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu.
Mimi nitakutangulia, na kuisawazisha milima mbele yako. Nitaivunjavunja milango ya shaba, na kuvikatakata vizuizi vyake vya chuma. Enyi watu wa mataifa mliosalia, kusanyikeni pamoja mje! Nyinyi mmekosa akili: Nyinyi mwabeba sanamu za miti na kumwomba mungu asiyeweza kuokoa watu. Semeni wazi na kutoa hoja zenu; shaurianeni pamoja! Ni nani aliyetangaza zamani matukio ya sasa? Ni nani aliyetamka mambo haya zamani? Je, haikuwa mimi Mwenyezi-Mungu? Hakuna Mungu mwingine ila mimi! Mimi ni Mungu wa haki na mwokozi; hakuna mwingine ila mimi. Nigeukieni mimi mpate kuokolewa, popote mlipo duniani. Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine. Mimi nimeapa kwa nafsi yangu, ninachotamka ni ukweli, neno langu halitarudi nyuma: Kila binadamu atanipigia magoti, kila mtu ataapa uaminifu. “Watasema juu yangu, ‘Haki na nguvu viko kwa Mwenyezi-Mungu peke yake.’” Wote waliomwakia hasira Mwenyezi-Mungu watamjia yeye na kuaibishwa. Lakini wazawa wa Israeli watapata ushindi kwake Mwenyezi-Mungu na kufurahi. Nitakupa hazina zilizofichwa gizani, na mali iliyo mahali pa siri, upate kutambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninayekuita kwa jina lako.
Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini.
“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni mlango, nanyi mtafunguliwa. Maana, yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye mlango hufunguliwa.
“Kama ningekuwa wewe ningemgeukia Mungu, ningemwekea yeye Mungu kisa changu, yeye atendaye makuu yasiyochunguzika, atendaye maajabu yasiyohesabika.
Huyu Mungu matendo yake hayana dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia usalama.
Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Je, mama aweza kumsahau mwanawe anayenyonya, asimwonee huruma mtoto wa tumbo lake? Hata kama mama aweza kumsahau mwanawe, mimi kamwe sitakusahau. Nimekuchora katika viganja vyangu; kuta zako naziona daima mbele yangu.
Hata hivyo niko daima nawe, ee Mungu! Wanishika mkono na kunitegemeza. Wewe waniongoza kwa mashauri yako; mwishowe utanipokea kwenye utukufu.
Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uhai.”
“Nitawaongoza vipofu katika njia wasiyoifahamu, nitawaongoza katika njia ambazo hawazijui. Mbele yao giza nitaligeuza kuwa mwanga, na mahali pa kuparuza patakuwa laini. Huo ndio mpango wangu wa kufanya, nami nitautekeleza.
Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.
kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe.
Nitabubujisha mito kwenye milima mikavu, na chemchemi katika mabonde. Nitaigeuza nyika kuwa bwawa la maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji.
Ee Mungu, wewe u Mungu wangu, nami nakutafuta kwa moyo; roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu; nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji. Watauawa kwa upanga, watakuwa chakula cha mbweha. Lakini mfalme atafurahi kwa sababu ya Mungu; wanaoahidi kwa jina la Mungu watamsifu, lakini vinywa vya waongo vitafumbwa. Nimetaka kukuona patakatifuni pako, niione nguvu yako na utukufu wako. Fadhili zako ni bora kuliko maisha, nami nitakusifu kwa mdomo wangu.
Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uhai na amani.
Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu.
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi, naam mimi, ndimi ninayekufariji. Kwa nini wewe unamwogopa mtu ambaye hufa, binadamu ambaye hutoweka kama nyasi? Wewe umenisahau mimi Mwenyezi-Mungu Muumba wako, niliyezitandaza mbingu, na kuiweka misingi ya dunia! Wewe waendelea kuogopa siku zote, kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu wako, kwamba yuko tayari kukuangamiza! Lakini hasira yake itafika wapi?
Wanionesha njia ya kufikia uhai; kuwako kwako kwanijaza furaha kamili, katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.