Walawi 12 - Swahili Revised Union VersionUtakaso wa wanawake baada ya kujifungua 1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na hao wana wa Israeli, uwaambie, Mwanamke akitunga mimba na kuzaa mtoto wa kiume, ndipo atakuwa najisi siku saba; kama katika siku za kutengwa kwake kwa ajili ya hedhi ndivyo atakavyokuwa najisi. 3 Siku ya nane mtoto atatahiriwa govi ya zunga lake. 4 Na huyo mwanamke atakaa muda wa siku thelathini na tatu ili kutakata damu yake. 5 Lakini kama amezaa mtoto wa kike naye atakaa muda wa siku sitini na sita ili kutakata damu yake. 6 Kisha hizo siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, kwa ajili ya mtoto wa kiume, au kwa ajili ya mtoto wa kike ataleta mwana-kondoo wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa, au hua, kuwa sadaka ya dhambi, awalete mlangoni pa hema ya kukutania, na kumpa kuhani; 7 na yeye atawasongeza mbele za BWANA, na kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atatakasika. Hii ndiyo amri yake huyo azaaye, awe ni mtoto wa kiume au wa kike. 8 Kama mali yake huyo mwanamke haimudu mwana-kondoo, hapo ndipo atakapochukua hua wawili, au makinda mawili ya njiwa; mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa, na wa pili kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya