Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mika 2 - Swahili Revised Union Version


Maovu ya jamii yashutumiwa

1 Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, sababu wana uwezo mikononi mwao.

2 Nao hutamani mashamba, na kuyanyakua; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake.

3 Basi BWANA asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya.

4 Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, Sisi tumeangamizwa kabisa; Yeye analibadili fungu la watu wangu; Jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu.

5 Kwa hiyo hamtakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa BWANA.

6 Msitabiri, ndivyo watabirivyo; wasiyatabiri mambo haya; lawama hazikomi.

7 Je! Litasemwa neno hili, enyi nyumba ya Yakobo, Roho ya BWANA imepunguzwa? Je! Haya ni matendo yake? Je! Maneno yangu hayamfai yeye aendaye kwa unyofu?

8 Lakini siku hizi mmeinuka kama adui za watu wangu; mnawapokonya joho lililo juu ya nguo za hao wapitao salama bila kutarajia vita.

9 Wanawake wa watu wangu mnawatupa nje ya nyumba zao nzuri; watoto wao wachanga mnawanyang'anya utukufu wangu milele.

10 Ondokeni, mwende zenu; maana hapa sipo mahali pa raha yenu; kwa sababu ya uchafu mtaangamizwa, naam, kwa maangamizo makubwa sana.

11 Mtu akienda kwa roho ya uongo, akinena maneno ya uongo, akisema, Nitakutabiria habari ya mvinyo na kileo; mtu huyu atakuwa nabii wao watu hawa.


Ahadi kwa mabaki wa Israeli

12 Hakika nitakukusanya, Ee Yakobo, nyote pia; Bila shaka nitawakusanya waliobaki wa Israeli; Nitawaweka pamoja kama kondoo katika zizi; Kama kundi la kondoo katika malisho yao; Watafanya mvumo kwa wingi wa watu;

13 Avunjaye amekwea juu mbele yao; Wamebomoa mahali, wakapita mpaka langoni, Wakatoka nje huko; Mfalme wao naye amepita akiwatangulia, Naye BWANA ametangulia mbele yao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo